KOCHA mpya wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Charles Boniface
Mkwasa amewataka mashabiki wa Simba kutomzomea pindi watakapomuona
kwenye mazoezi au mechi, kwa vile atakuwa pale kwa ajili ya kuangalia
maendeleo ya wachezaji wake wa timu ya taifa.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Mkwasa alisema mashabiki wanatakiwa
kufahamu kuwa yeye ni kocha wa taifa, hivyo atakuwa akitembelea katika
mechi za timu mbalimbali kuangalia wachezaji na maendeleo ya wale
wanaocheza timu ya taifa.
“Mashabiki wa Simba mnaponiona kwenye mechi zenu msinikimbize kwa
mawe mkadhani kuwa nimekuja kwa ajili ya Yanga, nitakuwa na utaratibu wa
kutembelea timu kuangalia wachezaji, mnajua kazi ya kocha wa taifa ndio
hiyo,” alisema Mkwasa ambaye pia ni Kocha Msaidizi wa Yanga.
Kujihami kwa Mkwasa ni kutokana na tabia iliyopo kwa mashabiki hasa
wa Yanga na Simba, pindi wanapoona kiongozi wa Yanga au Simba anakwenda
kwenye mechi zao hufanya vurugu.
Alisema atakuwa anachagua wachezaji wenye uwezo na ambao wanatumika
katika timu zao, na kwamba iwapo kuna baadhi watakuwa wanacheza timu ya
taifa na wakabainika viwango vyao vimeshuka watapigwa chini.
Alisema atakuwa akichagua wachezaji kwa kuangalia uwezo wake bila kubagua na sio timu, na kwamba wachezaji wanatakiwa kujituma.
Mkwasa alipewa jukumu la kuinoa Stars baada ya aliyekuwepo Mart Nooij
kutimuliwa kwa kufanya vibaya katika michuano ya kimataifa.
Benchi la ufundi la Taifa Stars kwa sasa linasimamiwa na makocha
wazalendo chini ya Mkwasa, msaidizi wake Hemed Morocco na mshauri wa
timu Abdallah Kibadeni.
Kitendo cha timu ya Taifa kupewa kocha mzalendo sio cha kwanza, miaka
ya nyuma aliwahi kuchukuliwa kocha wa Simba, James Singalaza.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment