Kitengo cha Mawasiliano cha CCM kimethibitisha
uwapo wa kikao hicho ambacho pia kitapitia orodha ya makada wa chama
hicho wanaowania urais.
Kikao hicho kitatanguliwa na kikao kingine cha
sekretarieti kinachofanyika leo ambacho kitaongozwa na Katibu Mkuu wake,
Abdulrahman Kinana.
Mpaka sasa, makada 40 wamejitokeza kuomba nafasi
ya kuipeperusha bendera ya CCM katika kiti cha urais, kwenye Uchaguzi
Mkuu Oktoba 25, wengi wanaendelea na kazi ya kukusanya wadhamini katika
maeneo mbalimbali ya nchi.
Juzi, wakati akizungumza na Televisheni ya Taifa
(TBC), Makamu Mwenyekiti wa CCM - Bara, Philip Mangula aligusia kidogo
juu ya wagombea urais na kusema atakayepitishwa hatajiuza mwenyewe, bali
atauzwa na chama hicho alichodai kuwa kina wanachama milioni saba nchi
nzima.
Chama hicho tawala kinakabiliwa na wakati mgumu wa
kupitisha jina la mgombea urais kutokana na idadi kubwa ya
waliojitokeza kuwania nafasi hiyo jambo ambalo halikujitokeza wakati wa
upitishwaji wa mgombea urais wa chama hicho mwaka 1995 na 2005.
Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa
huenda kikao hicho kikahudhuriwa na wajumbe wachache kutokana na
kuitishwa kwa dharura.
Ilieleza kuwa kuna nafasi zilizo wazi kutokana na
sababu mbalimbali, kuanzia ngazi za wilaya mpaka taifa na kwamba lazima
zijazwe katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu ili kila mtu
atimize wajibu wake.
“Kuna nafasi za makatibu na wenyeviti ambazo ziko
wazi kuanzia wilayani mpaka taifa. Kikao hicho kinakwenda kuzibainisha
na kisha kuzijaza,” kilieleza chanzo hicho.
Suala jingine litakalojadiliwa katika kikao hicho
ni mabadiliko ya uongozi katika nafasi ya Mhariri Mtendaji wa Gazeti la
Uhuru, Joseph Kulangwa ambayo imesababisha mgomo wa wafanyakazi
wanaopinga uamuzi huo. Gazeti hilo ni la chama hicho tawala.
Kwa mujibu wa ratiba ya chama hicho, Kamati ya
Usalama na Maadili itafanya kikao chake Julai 8 na kufuatiwa na Kamati
Kuu Julai 9 ambayo inatarajiwa kuchuja wagombea hao 40 na kupata watano
ambao majina yao yatawasilishwa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC)
itakayofanyika Julai 10 kuchuja wagombea hao na kubaki watatu
watakaopigiwa kura na mkutano mkuu kumpata mmoja. Mkutano huo mkuu
utafanyika Julai 11 na 12 .
0 comments:
Post a Comment