TIMU ya soka ya Simba jana asubuhi ilianza rasmi mazoezi ya Gym kwa
ajili ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara
inayotarajia kuanza kutimua vumbi mwezi wa nane mwaka huu.
Kocha msaidizi wa timu hiyo Selemani Matola, ndiye aliyesimamia
mazoezi hayo yaliyofanyika kwenye Gym iliyopo karibu na mataa ya Veta na
kuhudhuriwa na wachezaji tisa wengi wao wakiwa ni wale wa kikosi cha
pili.
Akizungumza na gazeti hili Matola, alisema wameanza taratibu kwa
ajili ya kuweka miili ya wachezaji wao sawa kutokana na mapumziko ya
muda mrefu na baada ya kukaa sawa watahamia uwanjani pamoja na ufukweni
ili kutengeneza nguvu kwa kikosi chao cha msimu ujao.
“Ninachofanya hapa ni kuiandaa miili yetu kwa ajili ya kazi
tumedhamiria kufanya kazi ndiyo maana leo tupo hapa na baada ya kuwasili
kwa Kocha Mkuu Dylan Kerr, kuanzia Jumatatu tutabadili mpangilio wa
mazoezi yetu,” alisema Matola.
Nahodha huyo wa zamani alisema hawezi kusema mambo mengi hivi sasa
kwa sababu timu ndiyo imeanza mazoezi siku ya kwanza, lakini
anafurahishwa na jitihada zinazofanywa na uongozi wa timu yake katika
kukiboresha kikosi chao cha msimu ujao.
Hadi hivi sasa Simba imekamilisha usajili wa wachezaji watatu ambao
ni Mohamed Faki, Peter Mwalyanzi na Samir Hajji Nuhu huku wachezaji
Leodit Mavugo na Paol Kiongera nao wakitajwa kuongezwa kwenye usajili wa
msimu ujao.
Wachezaji waliohudhuria kwenye mazoezi ya jana asubuhi ni Mohamed
Hussein ‘Tshabalala’, Said Ndemla, Awadhi Juma, Denis Richard, Mussa
Hassan ‘Mgosi’, Issa Abdallah, Mbaruku Yusufu, David Kisu na Hassan
Kessy.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment