Mdahalo wa kwanza ulikuwa ufanyike Jumatatu
wiki hii, lakini ukashindikana kutokana na waliojitokeza kuwania urais kupitia
CCM na ambao walithibitisha kushiriki, hawakutokea wote na hivyo kusababisha
usifanyike.
Waalikwa kwenye mdahalo huo wameshaeleza
sababu za kutohudhuria kwao, hasa wakiegemea kukanganywa na kauli mbili tofauti
zilizotoka kwa viongozi wao kuhusu msimamo wa chama na pia kubadilika kwa
ratiba kulikosababisha waendelee na mipango mingine, hasa wakati huu ambao
wanazunguka mikoani kutafuta wadhamini.
Ni sababu za msingi ambazo zinaeleweka.
Inapotokea kiongozi mmoja anawakataza kushiriki midahalo hiyo kwa maelezo kuwa
chama hakijapata mgombea urais, na saa 24 baadaye kiongozi mwingine akasema
wahudhurie, ni lazima kauli hizo zitawachanganya na kusababisha waamue
kuendelea na mipango mingine ili wasipoteze muda wakati huu muhimu kwao.
Lakini tunachotaka kueleza hapa si kufanyika
au kutofanyika kwa mdahalo huo, bali umuhimu wa fursa hiyo katika kipindi hiki
cha kuelekea kupiga kura kuamua maisha ya Watanzania yachukue sura gani kwa
miaka mitano ijayo na kwa mtazamo mpana zaidi, kwa mustakabali wa maisha yao
yote ya baadaye.
Kwa maana hiyo, uchaguzi wa Rais ni tukio
muhimu kwa mustakabali wa Taifa hivyo ni lazima wananchi wafanye uamuzi sahihi
wakati wa kupiga kura. Uamuzi sahihi utawezekana tu ikiwa wapigakura watapata
fursa ya kutosha ya kuwasikia waomba urais, kuchambua hoja zao na kuwauliza
maswali ili waone jinsi wanavyoweza kuzitetea hoja zao.
Moja ya njia za kuwawezesha kuonekana na
kusikika ni kwa kushiriki katika midahalo ya wazi ambako watajieleza waziwazi,
kuelezea vipaumbele vyao na kutetea hoja zao kabla ya wananchi kwenda kwenye
sanduku la kura Oktoba 25.
Tunaamini kuwa wagombea wana wajibu wa
kushiriki kwenye midahalo hii ili waeleze sera zao kwa jamii wanayotaka
kuiongoza na baadaye kuulizwa maswali na kuyajibu ili waonyeshe ukomavu wao na
jinsi walivyojipanga si tu kuliongoza Taifa hili, bali kulitoa katika hali
fulani na kulipeleka kwenye hali nyingine.
Kwa vipindi viwili sasa, Tanzania
haijashuhudia midahalo hii tangu wagombea wa mwaka 1995, Benjamin Mkapa,
Augustine Mrema na Profesa Ibrahim Lipumba waliposhiriki mdahalo ambao uliwapa
wananchi fursa nzuri ya kuwajua waliokuwa wanataka kuwaongoza na hatimaye
kufanya uamuzi wakiwa na ufahamu tosha.
Hatuamini kuwa hali hii ya kuwanyima fursa
wapigakura kuwajua vizuri wagombea wao wa urais, itajitokeza kwenye Uchaguzi
Mkuu wa safari hii ambao umekuja wakati kuna mwamko mkubwa wa kisiasa na
wananchi kukomaa zaidi kiasi kwamba kuna kila umuhimu kwao kuwasikia wagombea
wao ili wafanye uamuzi sahihi. Mgombea ambaye hatataka kushiriki kwenye
midahalo hii, ana ajenda ya siri na hivyo hafai kupewa uongozi wa nchi kwa kuwa
hataki kulishirikisha ajenda yake.
Vyama visiwazuie makada wake kushiriki kwenye
midahalo kwa kuwa vitakuwa vinawanyima wapigakura fursa ya kuwajua vizuri
wagombea na pia kuwanyima haki ya kufanya uamuzi sahihi, huru na wa haki.
0 comments:
Post a Comment