Katika Mkoa huo ambao ni wa 31, Lowassa alipata wanachama 100,438 waliomdhamini.
Kanali Mwisongo alisema tangu alipojiunga na Tanu mwaka 1967 ambayo
sasa ni CCM, hajawahi kumsikia hayati Mwalimu Nyerere akitamka neno la
namna hiyo na amekuwa akihudhuria vikao vyote kuanzia Halmashauri Kuu ya
CCM (Nec), Kamati Kuu na Mkutano Mkuu.
“Mimi nimekuwa katika vikao hivyo vyote na kama Nyerere ukikosea au
hakutaki, alikuwa anakukataa waziwazi na pia unatangazwa kwenye vyombo
vya habari. Lowassa ni mtu anayewapenda Watanzania tangu zamani,”
alisema Kanali Mwisongo.
Alitolea mfano wa mwekezaji aliyedai kuwa aliletwa na mmoja wa
`wakubwa ' ili ajenge hoteli katika chanzo cha gesi, lakini Lowassa
aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa wakati huo,
alikataa.
“Alikataza hoteli kujengwa katika chanzo cha gesi kwa manufaa ya
Watanzania na kila alichoamua aliamua kwa manufaa ya Watanzania,”
alisema Kanali Mwisongo.
Aidha, aliwaonya viongozi wa chama hicho kuacha kutoa matamshi
kabla ya vikao havijakaa kwani ni makosa makubwa na wanasababisha CCM
kuyumba kama hakina mwenyewe.
“CCM kimeyumba kupita kiasi kutokana na hawajui msemaji mkuu ni
nani na vikao vikuu vinakaa saa ngapi vya kuamua hayo yanayosemwa ovyo.
Viongozi wasifanye makosa katika Kamati Kuu, Kamati ya Maadili ambako
kutakuwa na mizengwe, lakini watambue Nec ina nguvu,” alisema Kanali
Mwisongo.
Naye Kada mwingine mkongwe, Dk. Juma Ngasongwa, ambaye amewahi kuwa
Waziri katika awamu mbalimbali, alisema viongozi wa CCM wameyumba siku
za karibuni kutokana na kusemana hadharani wenyewe kwa wenyewe na
Lowassa ndiye dawa ya kuondoa maneno hayo.
“Kuna wanachama wengi wamehamia vyama vingine kutokana na kushindwa
kuongoza CCM. Sasa huko katika vyama vingine watawezaje kuviongoza? CCM
irudishe wana-CCM imara madarakani ambaye ni Lowassa,” alisema Dk.
Ngasongwa.
Kwa upande wake, aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Steven
Mashishanga, alisema vikao vinavyotarajiwa kukaa hivi karibuni
vihakikishe vinatenda haki kwa kuangalia ni nani aliye na alama nyingi
za vyema mgongoni na anayehitajika na wengi.
Alisema Lowassa ni kiongozi pekee mwenye uwezo na sifa za kuwa Rais kwani amekitumikia chama kwa miaka mingi.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Fikiri Juma,
alimtaka Nape Nnauye, kuacha kutoa kauli kuwa wananchi wengi wamepewa
fedha kwa ajili ya kumdhamini Lowassa wakati wapo wagombea wengi
wamefika kuomba udhamini na kutoa rushwa.
Alisema hakuna mtu aliyepewa fedha kwa ajili ya kumdhamini Lowassa,
bali ni wananchi wenyewe ndiyo wana maamuzi ya mwisho ya kumchagua
kiongozi wanayemtaka na si Nape.
“Haki isipotendeka katika vikao vya maamuzi sisi bado tupo pamoja
na wewe, katika semina ya wenyeviti tuliyopewa tuliambiwa tuchague
viongozi wanaokubalika ndani na nje ya Chama ambaye ni wewe,” alisema
Juma.
Akizungumza na wanachama CCM, Lowassa aliwashukuru kwa kumdhamini na kwamba Mkoa wa Morogoro amepata watu wengi.
Hata hivyo, alisema licha ya kupata wadhamini wengi, atapeleka
wanaotakiwa CCM na wengine atawahifadhi nyumbani kwake kama kumbukumbu
yake.
Lowassa amepata jumla ya wadhamini 863,479 katika mikoa 31 aliyoitembelea.
Aidha, alitaja sababu za kugombea urais kuwa ni pamoja na kuchoshwa
na hali ya umaskini na pia Rais Jakaya Kikwete, anamaliza muda wake wa
uongozi hivyo anatakiwa kukabidhi kijiti kwa mtu mwingine.
"Na anayeweza kukipokea kijiti hicho na kuyaendeleza yale
aliyoyaacha Rais Kikwete, ni mimi. Kazi hii haipatikani hivi hivi,
naomba dua zenu Waislamu na Wakristo ni muhimu sana,” alisema Lowassa.
Alisema endapo atafanikiwa kupata nafasi anayoiomba, kwanza atahakikisha anafufua viwanda katika mji wa Morogoro.
Aidha, alisema anasononeshwa mno na migogoro ya wakulima na
wafugaji kwa hiyo atakapoingia madarakani, ataunda tume ya kusuluhisha
migogoro hiyo.
Aliwataka Watanzania wajiandae kuwa na `spidi' ya kuchapa kazi
kwani anataka mchakamchaka wa Maendeleo na atakayeshindwa atalazimika
kukaa pembeni.
0 comments:
Post a Comment