Image
Image

Ramadhan iwajenge waumini kiimani.


Kuanzia jana, waumini wa Kiislamu nchini waliungana na wenzao duniani kote kuanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Saumu ya Ramadhan kama ilivyo maarufu kwa waumini wa dini hiyo, ni moja ya nguzo tano za Uislamu inayotekelezwa na waumini kwa minajili ya kuwajenga kuwa wacha Mungu.
Nguzo nyingine ni kutoa shahada, kusimamisha swala, kutoa zaka na kuhiji katika mji mtukufu wa Makka.
Tunapotoa salamu zetu za Saumu njema tukitambua kuwa hizi ni siku 29 au 30 za heri na kuchuma mema kama mafunzo ya dini ya Kiislamu yanavyosisitiza. Hivyo, tunalazimika kuwakumbusha waumini wa Kiislamu kushikamana vilivyo na mafunzo haya ili hatimaye iwe sababu ya wao kupata fadhila zinazotokana na kutekeleza ibada hii adhimu.
Tukitambua kuwa ndani ya mwezi huu, waumini wanasisitizwa kufanya mambo mema na mambo mbalimbali ya heri kwa lengo la kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, ni vyema basi waumini hawa wakatambua kuwa wana wajibu mkubwa wa kuendeleza wanayofanya sasa hata katika miezi mingine.
Kama ndani ya mwezi huu, waumini wanayapa kisogo maovu mbalimbali kama wizi, uzinzi, ulevi, uasherati, husuda, kusema uongo, usengenyaji na mengineyo na kushitadi katika mema kama swala, kusoma Quran, kufanya dhikri na kusaidia wasio na uwezo, hatuoni sababu kwa nini mwenendo huu wasiuendeleze hata baada ya kumalizika kwa Saumu.
Matunda ya kufanya mema siyo tu yanasaidia kupata fadhila na kuwajengaa kiimani kama inavyoelezwa na mafunzo mbalimbali ya dini yao, pia kutawafanya kuendelea kuwa raia wema ndani ya jamii na nchi kwa jumla.
Aidha, tunapowahimiza waumini wa Kiislamu kujitanibu na maovu na kujikurubisha na mema, tutumie nafasi hii pia kuwakumbusha baadhi ya watu hasa wafanyabiashara wa vyakula kuacha kutumia mwezi huu kama fursa ya kujineemesha kiuchumi.
Uko ushahidi kuwa baadhi ya wafanyabiashara huwa wanapandisha, kwa makusudi, bei ya bidhaa, ambazo hutumiwa kwa wingi na waumini ndani ya mfungo. Wanaoathirika na hali hii siyo waumini wa Kiislamu pekee, bali hata wananchi wengine.
Kinachosikitisha zaidi, baadhi ya wafanyabiashara hawa wamo waumini wa Kiislamu ambao kwa upande mmoja wanajigubika vazi la mema ya Saumu, lakini kwa upande mwingine wanajivika vazi la maovu.
Wasichoelewa waumini hawa ni kuwa mafunzo ya Uislamu yanasisitiza mtu kuifuata dini kwa ukamilifu wake na siyo kwa mtindo wa kuchagua amali za kutenda.
Kwa mfano, Uislamu unaohimiza haki, uaminifu msikitini ndiyo huohuo unaohimiza mambo hayo kufanywa katika maisha ya muumini nje ya msikiti, ikiwamo kwenye miamala mbalimbali ya kibiashara na maisha kwa jumla.

Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment