Kati ya fedha hizo, Sh444.6 bilioni kwa ajili
ya miradi ya maendeleo na Sh369.3 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Kimsingi afya ni sekta mojawapo yenye changamoto lukuki hapa nchini. Ni sekta
muhimu katika kuchangia ustawi wa Taifa. Kumekuwa na changamoto
kadhaa katika sekta ya Afya. Hata hivyo Serikali imefanya jitihada
kubwa kukabiliana na changamoto hizo.
Baadhi ya jitihada hizo ni
kupandisha viwango vya hospitali, kukarabati na kuongeza majengo, kuongezeka
kwa wataalamu wa afya pamoja na huduma za kitaaluma katika baadhi ya
hospitali zetu.
Lakini pamoja na jitihada hizo mabadiliko
hayo yamekuwa hayalingani na ongezeko la idadi ya watu pamoja na sayansi
na teknolojia. Kwa mfano tatizo la uhaba wa dawa limeendelea kuvikumba
vituo vyote vya Serikali hapa Tanzania kiasi cha kuwa chanzo cha vifo
vingi ambavyo vinatibika.
Tatizo jingine katika sekta hiyo ni upungufu
wa vifaa tiba. Vituo vingi vya tiba vimekabiliwa na upungufu huo na
kusababisha wagonjwa kutopata tiba kwa ufasaha hivyo kuhatarisha afya zao. Si
ajabu hospitali kukaa muda mrefu bila kipimo cha wingi wa damu, kipimo cha
sukari na hata X-Ray.
Uhaba wa dawa umekuwa ni tatizo kubwa nchini
na malalamiko mengi yametolewa. Kwa mfano mapitio ya kumbukumbu za Bunge ya
2008/09-2012/13 yanaonyesha takribani asilimia 35 ya wabunge ambao huchangia
katika mjadala wa bajeti ya afya, hulalamika uhaba wa dawa vituoni na kuitaka
Serikali kuongeza fedha.
Pia kuna tafiti kadhaa zimefanywa kuhusu
tatizo la uhaba wa dawa kwenye hospitali na vituo vya afya. Kwa mfano utafiti
uliofanywa na Taasisi ya Ifakara nchini (IHI), ulibaini kuwa katika
kipindi cha mwaka 2012 dawa muhimu zilizokuwepo katika vituo zilikuwa asilimia
41 tu.
Kwa mujibu wa utafiti huo, hali hiyo
ilimaanisha kuwa kwa takribani asilimia 60 ya dawa muhimu hazikuweza kupatikana
katika vituo vya huduma za afya. Katika utafiti huohuo, ilibainika kuwa dawa za
antibiotics zilipatikanna kwa asilimia 57 tu, kitu ambacho ni hatari
sana kwa magonjwa ya milipuko ambayo yamekuwa yakisababisha vifo.
Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Dk Antony
Mbassa katika hotuba bungeni jana alizungumzia suala la uhaba wa dawa katika
hospitali nyingi nchini, na kufafanua kuwa takwimu za Shirika la Afya
Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa upatikanaji wa dawa katika vituo vya Serikali ni
asilimai 24 na vituo binafsi ni asilimia 47.
Kuna matatizo mengi katika sekta ya afya
ambayo hatuwezi kuyaorodhesha yote hapa, lakini kubwa zaidi ni ufinyu wa bajeti
kwa sekta hii muhimu. Mbali na ufinyu, hata hizo fedha kidogo zinazopelekwa,
hazifiki zote. Hali hiyo inafanya suala la afya bora kuwa gumu na hivyo kujenga
fikra kwamba iko siku itakuwa vigumu kumpata Mtanzania mwenye afya bora.
Kwa hali hiyo ni dhahiri kwamba kuna kila
sababu kwa Serikali kuelekeza nguvu zake kwenye sekta ya afya. Bila kuwa na
Watanzania wenye afya bora, ni nadra kuwa na taifa lenye nguvu kazi madhubuti.
Wito wetu na kuitaka Serikali kutochezea sekta hii muhimu kwa ustawi wa Taifa.
0 comments:
Post a Comment