Mtandao wa Wanawake na
Katiba Tanzania utashawishi wanawake nchini na wale wa makundi ya pembezoni
kutounga mkono chama chochote cha kisiasa kisichotetea ajenda ya kuinua maisha
na kulinda utu wa wanawake, ambacho hakitaonyesha ari ya dhati ya kuteua
wanawake kuwania nafasi mbalimbali wakati wa uchaguzi na kile ambacho viongozi
wake wanadharau haki ya msingi ya kujenga usawa wa jinsia.
Mtandao huu
unaounganisha asasi za kiraia takriban 65 na watu binafsi watetezi wa haki za
wanawake, watoto na makundi yaliyoko pembezoni, umekuwa ukifuatilia mwenendo wa
vyama vya siasa hasa kwa wanaotangaza nia ya kugombea uongozi katika ngazi ya
uraisi, ubunge, baraza la uwakilishi na udiwani na kubaini kuwa baadhi ya vyama
vimeshindwa kuteua wanawake kuwania nafasi mbalimbali ndani ya nchi.
Katika ufuatiliaji huo,
Mtandao wa Wanawake na Katiba umepata wasi wasi wa kutokuwepo kwa watangaza nia
wanawake wala kusikika kwa ajenda ya kuimarisha ukombozi wa kimapinduzi wa
wanawake wakati huu wa hatua za awali za uteuzi wa viongozi wa kisiasa ndani ya
vyama.
Aidha Mtandao
umebainisha kutokuwepo uzingatiaji wa misingi inayopelekea kuwepo kwa usawa wa
jinsia katika mchakato wa kuteua wagombea ndani ya vyama vya siasa ambavyo
vimeshateua wagombea ambapo hakuna hata mwanamke mmoja aliyeteuliwa.
Mtandao
umeliona jambo la kutoteuliwa kwa wanawake katika ngazi za awali ndani ya vyama
ni kinyume cha msingi wa kujenga, kukuza na kuimarisha demokrasia ya
chama na nchini kwa ujumla.
Mtandao umewataka
viongozi na wanachama wa vyama yva siasa, na wale wanaotangaza nia kubeba
ajenda ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi katika
kupambana na masuala yanayowagusa moja kwa moja yakiwemo kutokulindwa kwa utu
wao, kuondoa ukatili wa kijinsia, kupinga mila
potofu kama vile ukeketaji na ndoa za utotoni, umiliki wa raslimali za nchi,
pamoja na suala zima la kuhakikisha kuwa wanawake wanapata haki sawa katika
nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Valerie N. Msoka
Mkurugenzi Mtendaji
0 comments:
Post a Comment