Sheria zisimamiwe kudhibiti uuzwaji holela wa dawa.
Chama cha Wafamasia (PST) juzi kilitoa taarifa kuhusu matumizi mabaya ya dawa yanayosababishwa na kuwapo kwa maduka holela ambayo hutoa dawa bila kuzingatia kanuni , maadili na taratibu za kitabibu na matokeo yake ni kuzorotesha afya za wananchi.
PST ilisema kuwa tabia ya watu kununua dawa kiholela bila ya kuwa na cheti kinachoonyesha maelekezo ya daktari husababishwa na maduka hayo ambayo wamiliki wake si waadilifu na wanajali zaidi biashara kuliko taaluma yao.
Ilisema kuwa baadhi ya madhara ya tabia hiyo ni maduka hayo kufikia hatua ya kuuza dawa za kutolea mimba, jambo ambalo linaweka rehani maisha ya watu wengi hasa wasichana wadogo.
Kwa mujibu wa PST matatizo hayo yote yanatokana na kutokuwapo kwa usimamizi mzuri wa sheria zinazoongoza uanzishwaji na utendaji wa maduka hayo na kusababisha wamiliki kuyaendesha kwa kujali fedha zaidi badala ya afya za wateja wao, taratibu na kanuni.
Sheria za uanzishwaji wa maduka hayo zipo na zinasisitiza kuwa ni lazima yasajiliwe, yawe na mtaalamu wa masuala ya famasia, na yawe yanauza baadhi ya dawa za moto kwa kufuata maelekezo ya daktari yaliyoandikwa kwenye cheti cha mteja.
Lakini kwa mujibu wa PST, sheria na kanuni hizo hazifuatwi. Badala yake maduka yanaanzishwa kiholela kwa wanaoomba kuyafungua kuwasilisha nyaraka tu kuonyesha wameajiri wafamasia, kumbe wametuamia vyeti.
Ukaguzi wa uendeshaji wa maduka hayo hufanywa kwa operesheni badala ya suala hilo kuwa la kila mara ili kujenga nidhamu ya kuheshimu sheria. Matokeo ya ukaguzi wa kioperesheni ni kushindwa kuwanasa wanaokiuka sheria kwa kuwa hutarifiana kuwa kuna operesheni na kuwamua kutoyafungua.
Mbali na kuuza dawa hatari kama za kutolea mimba, maduka hayo yamekuwa yakikutwa na dawa ambazo hazijaidhinishwa kuuzwa nchini na nyingine ambazo muda wake wa matumizi umekwisha.
Matokeo ya vitendo hivyo ni kuweka rehani afya za Watanzania. Watu ambao wanatakiwa tiba sahihi ili watibu magonjwa yao, wanakwenda kwenye maduka ya dawa na kuzinunua bila ya kuonana na madaktari ili wapewe maelekezo sahihi na matokeo yake ni kufuga zaidi magonjwa na vijidudu kuwa sugu.
Hata kama wagonjwa hao wanauziwa dawa kwa maelekezo ya madaktari, lakini zinaweza kuwa ni zile zilkizokwisha muda na matokeo yake huwa ni kuvifanya vijidudu kuwa sugu na magonjwa kuwa shida kutibika.
Ushauri wetu ni kwa Serikali na wahusika wote kuwa makini katika kusimamia uanzishwaji na uendeshwaji wa maduka haya muhimu, hasa kwa kuzingatia kuwa ndiyo yanahudumia wananchi kwa karibu zaidi kwa kuwa yapo kwenye makazi yao.
Watu wanaotakiwa kuwa wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara wanatakiwa wasimamiwe ili wafanye kazi hiyo muhimu ya kuhakikisha kila duka lina mfamasia, dawa zilizopo ni zile zinazoruhusiwa, hazijaisha muda na kuhakikisha dawa zinazotolewa kulingana na maelekezo ya daktari.
0 comments:
Post a Comment