Image
Image

Shule za msingi za bweni na athari za kimalezi.


Hivi karibuni, serikali ya Rwanda imepiga marufuku shule za bweni kwa wanafunzi wa elimu ya msingi. 
Wizara ya Elimu ya nchi hiyo, imetoa muda wa miaka mitatu kwa shule za msingi za bweni kufunga huduma hiyo.
Lengo la Serikali ya Rwanda ni kutaka kuona watoto wakipata muda zaidi wa kukaa na wazazi wao, kuwafinyanga kimalezi mpaka wafikie umri wa kujitambua zaidi.
Hivyo kwa serikali ya Rwanda muda mwafaka wa wanafunzi kwenda  shule za bweni ni  pale wanapofika sekondari.
Upepo wa shule za bweni kwa wanafunzi wenye umri mdogo umeikumba pia Tanzania. Hivi sasa kuna idadi kubwa ya shule zinazopokea wanafunzi chini ya miaka 10 wanaosoma elimu ya msingi. Je, ni mwafaka kwa Serikali ya Tanzania kufuata nyayo za Rwanda kuzuia shule hizo?
Utengano na wazazi
Hapa nchini, wanafunzi wanatumia miezi si chini ya tisa wakiwa shuleni, muda ambao   Meneja wa utafiti na uchambuzi wa sera wa shirika la HakiElimu, Godfrey Boniventure anasema hauwapi watoto nafasi ya malezi kutoka kwa wazazi
“Miezi tisa ni mingi kwa  mtoto kuwa mbali na malezi ya wazazi, kwa hivyo nakubaliana na mabadiliko ya Rwanda; ingetokea  hapa nchini ingesaidia  japokuwa ninaamini haiwezekani kutokana na changamoto ya umbali wa shule nyingi  zilivyojengwa  ambazo  zinalazimisha kuwa na bweni japo si vizuri kimalezi,’’ anasema na kuongeza:
“Kiuzoefu, watoto wengi  wanaosoma shule za bweni huathirika kimalezi; wanabadilika tabia bila mzazi kujua lakini kama mwanafunzi anakwenda shule na kurudi, ni rahisi kwa mzazi  kutambua mabadiliko na mwenendo wake.”
Anasema hata Korea Kusini ni miongoni mwa mataifa yaliyoendelea, lakini hayatumii mfumo wa shule za bweni ila kwa wanafunzi maalumu, kama anavyofafanua:
“Korea Kusini wanatumia shule za bweni kulea vipaji na si kwa masomo ya sekondari au shule ya msingi, vipaji ndiyo vinalelewa, kukuzwa ili kulinda visipotee.’’
Katibu Mkuu wa Umoja wa wamiliki wa shule na vyuo binafsi nchini (Tamongsco), Benjamin Nkonya, anasema uamuzi wa kufungia shule za bweni  kwa daraja la elimu ya msingi ni sahihi.
“Kuanzia kidato cha kwanza mpaka vyuoni inawezekana kukaa bweni na kwa Tanzania tunaweza kufanya hivyo, lakini lazima kuwapo na huduma nzuri za usafiri wa mabasi ya wanafunzi kwa wanafunzi wa shule za kwenda na kurudi nyumbani,’’anasema.

Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment