Image
Image

TFF yafunika kombe.


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limeamua kufunika kombe kunusuru aibu iliyokuwa itokee kuhusu sakata la mkataba kati ya Simba na mchezaji Ramadhani Singano ‘Messi’ kwa kuwataka wakutane na kuingia mkataba mpya.
Pande hizo mbili zilikutanishwa jana kufuatia kutokea mgogoro mkubwa baina yao, baada ya Messi kudai mkataba wake wa miaka miwili uliokuwa umalizike mwezi ujao umechezewa na Simba, ambao wanadai unamalizika Julai, mwakani.
Kikao hicho kilichofanyika jana kuanzia saa mbili hadi saa nane mchana, kilihudhuriwa na Messi, viongozi wa Chama cha Wachezaji Nchini (SPUTANZA) na mjumbe wa kamati ya utendaji ya Simba, Collins Frisch, huku mwongozaji akiwa Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa, kilifikia makubaliano hayo, ambayo kwa msemo wa Kiswahili unaweza kusema wameamua kufunika kombe mwanaharamu apite.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Mwesigwa alisema, wameamua kwa pamoja kuwa waachane na mkataba huo uliopita na waingie makubaliano mapya.
“Hiki kikao hakikuwa cha kuangalia nani ana makosa, tuliitisha ili kulisuluhisha suala hili na kwa kuwa mkataba huu aliingia mchezaji na uongozi uliopita, basi tumeamua waachane nao na wafanye makubaliano mapya, hivyo wasianze kujadili mkataba uliopita.
“Siwezi kusema ni mkataba gani ambao umeonyesha kuwa na makosa, hiyo ni siri na hayo tuliyoyaamua ndio maamuzi yetu kwa pamoja na wote tumeweka saini makubaliano hayo, ila nawataka wachezaji kuwa makini na mikataba wanayotaka kuingia na timu wahakikishe wanaisoma kwa umakini ili kuepusha mambo haya,” alisema Katibu huyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SUPTANZA, Mussa Kisoky, alisema waliamua kulipeleka TFF suala hilo kwa ajili ya kupata ufafanuzi pekee na ndio huo uliotolewa.
“Hatujawahi kusema kuwa mkataba umeghushiwa, lakini tulitaka TFF watupe ufafanuzi, tunatambua kuwa Messi ni mchezaji halali wa Simba na wanaweza kukaa na kufanya makubaliano mapya,” alisema.
Kwa upande wake, Messi alisema anamuachia Mungu maamuzi hayo yaliyofanywa na TFF kwani ndiye anayejua ukweli ni upi.
“Siwezi kusema kama nimeridhika au sijaridhika, lakini namuachia Mungu, najitambua kama mchezaji huru na nitafanya kama walivyosema TFF kuwa tufanye makubaliano mapya, nitawapelekea dau langu kama wakishindwa nitarudi tena hapa kuwaeleza.
“Najiuliza na nimewauliza kwenye kikao, je, nikipata ofa mazungumzo yatafanywa chini ya klabu ya Simba au mimi pekee, ila jibu lake sijalipata zaidi ya kuambiwa kuhusu mkataba huo mpya,” alisema.
Alisema, anaweza kuendelea kuichezea Simba kwa sababu hiyo ndio kazi yake, anaishukuru klabu hiyo kwa kumfikisha hapo alipo, lakini kuna wakati unafika anahitaji mabadiliko.
Sakata kama hili la Messi linalohusisha mkataba, liliwahi kumkuta mchezaji Athuman Idd ‘Chuji’ mwaka 2007/2008, wakati akitaka kuihama klabu hiyo na lilifika hadi kwenye vyombo vya dola kuchunguzwa, kutokana na madai ya Chuji kuwa saini yake ilikuwa imeghushiwa katika mkataba wake.
Wakati huo huo, uongozi wa Simba umeeleza kuwa kwa sasa hawatatoa tamko lolote kuhusu uamuzi uliofikiwa kwenye kikao hicho, umedai kikao cha Kamati ya Utendaji kitakachokaa leo jioni ndicho kitapitia uamuzi huo.
“Kamati ya Utendaji ya Simba kesho jioni (leo) inakutana kujadili pamoja na mambo mengine, uamuzi na mapendekezo ya kikao cha pamoja kati ya TFF, Simba na mchezaji Ramadhan Singano. Hakutakuwa na tamko lolote rasmi la klabu kabla ya kikao hicho,” ilisema taarifa iliyotumwa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya timu hiyo, Haji Manara.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment