Thamani ya Shilingi inazidi kuporomoka kadri siku zinavyokwenda
na kusababisha bei za bidhaa mbalimbali kuendelea kupaa bila ya kuwapo
na maelezo yoyote ya mkakati wa kudhibiti hali hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) ya kipindi kinachoishia Aprili, thamani ya Shilingi iliporomoka
hadi kufikia Sh1,815 kwa Dola 1 ya Marekani kulinganisha na Sh1,798.4
dhidi ya Dola moja kwa mwezi uliotangulia.
Maelezo ya kuporomoka huko kwa Shilingi yamekuwa
ni mepesi tu kwamba Dola inazidi kuimarika kutokana na uchumi wa
Marekani kuendelea kukua na pili ni nchi yetu kutouza bidhaa nyingi nje
ya nchi na badala yake inaagiza bidhaa nyingi, hali inayofanya mahitaji
ya Dola kuwa makubwa kuliko ya Shilingi.
Kwa mujibu wa takwimu hizo za BoT, kiwango cha
kuporomoka kwa thamani ya Shilingi kwa mwaka kilifikia asilimia 10.8
kutoka Sh1,637.7 kwa Dola moja ya Marekani ilivyokuwa Aprili mwaka jana.
Wakati thamani ya Shilingi ikizidi kuporomoka, bei
za bidhaa zinazidi kuongezeka kiholela mitaani na sababu kubwa
inayotolewa na wafanyabiashara imekuwa ni thamani ya Dola kuzidi kupaa.
Hivi sasa, shati ambalo mwaka jana lilikuwa likiuzwa kwa Shilingi
30,000, sasa linauzwa kati ya Sh40,000 na 45,000.
Maelezo yamekuwa ni rahisi tu kwamba thamani ya
Dola inazidi kupaa wakati Shilingi inazidi kwenda chini. Bei za vyakula
sokoni zinazidi kwenda juu, licha ya takwimu kuonyesha kuwa kiwango cha
mfumuko wa bei kuonekana kuwa kidogo.
Tatizo kubwa tunaloliona kwa viongozi wetu ni
kuridhika na maelezo hayo mawili kuwa kupanda kwa thamani ya Dola
kunasababishwa na kukua kwa uchumi wa Marekani na nchi kununua bidhaa
nyingi kutoka nje kulinganisha na zile inazonunua.
Haya ni maelezo mazuri lakini ambayo hayasaidii wananchi kuondokana na matatizo wanayoyapitia sasa.
Katika bajeti, kuna mikakati mingi ya muda mrefu
ya kuimarisha thamani ya Shilingi ambayo mwananchi wa kawaida hawezi
kunufaika nayo kwa wakati huu ambao anateseka kwa kupanda bei za vyakula
na bidhaa mbalimbali.
Ada za shule na vyuo sasa zinapangwa kwa kutumia
Dola kwa kuwa Shilingi inayumba, ada za pango za majengo ya ofisi,
malazi, bei za huduma mahotelini na sehemu nyingi zote zinapangwa kwa
kutumia dola, lakini kipato cha mwananchi hakipangwi kwa Dola na matokeo
yake ni mlalahoi kuendelea kuumizwa na kuporomoka kwa thamani ya
Shilingi.
Tunadhani Serikali inatakiwa ije na mpango kabambe
wa muda mfupi wa kuhakikisha inakabiliana na suala hilo kwa sasa ili
kuwapunguzia wananchi mzigo na pia kuja na mpango wa muda mrefu
kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi.
Kwa mujibu wa maoni ya wabunge wakati wa mjadala
wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2015/16, kuna bidhaa nyingi
zinazonunuliwa nje ya nchi ambazo zinapatikana au zinaweza kupatikana
hapa nchini.
0 comments:
Post a Comment