Ratiba ya uandikishaji ya NEC imelipatia jiji
la Dar es Salaam siku 13 za kuandikishaji wapigakura kwa kutumia teknolojia ya
Biometric Voters Registration (BVR).
Siku hizo ni pungufu kwa wastani wa siku 16
zilizotumika kwenye mikoa mingine nchini ambayo mingi ina nusu ya idadi ya watu
wenye umri wa kupiga kura ikilinganishwa na jiji la Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi Mosena
Nyambabe aliliambia gazeti hili kuwa ili NEC iendane na kasi ya muda uliopo,
inatakiwa kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha inakamilisha uandikishaji
wapigakura na ugawaji wa mipaka ya majimbo.
“Uzuri wa Dar es Salaam ni makao makuu ya
kila kitu, tutaangalia mwenendo wa uandikishaji kujua unafanyika kikamilifu au
la na utatupa picha hali ilikuwaje katika mikoa mingine. Bado wana kazi kubwa
kwa sababu hawajakamilisha kuchora ramani ya mikoa na majimbo…lazima wafanye
kazi ya kutisha,” alisema Nyambabe.
Alisema kazi ya mwaka mmoja na nusu haiwezi
kufanyika ndani ya wiki mbili ndiyo maana wakati mwingine huwa wanaona mipango
ya NEC kama viini macho. Hata hivyo akasema angalau sasa NEC wamejikita katika
Uchaguzi Mkuu kuliko Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Takwimu zinasemaje?
Takwimu za Shirika la Takwimu la Taifa (NBS)
za makadirio ya watu wenye sifa ya kupiga kura zinaonyesha kuwa Dar es Salaam
ina zaidi ya watu 2.93 milioni, idadi ambayo ni sawa na jumla ya wapigakura
katika mikoa sita ya Katavi, Lindi, Shinyanga, Njombe, Iringa na Rukwa ambao
wanakadiriwa kuwa 2.94 milioni.
NBS inakadiria Morogoro kuwa na wapigakura
zaidi ya 1.28 milioni wakati Tanga ina watu zaidi ya 1.12 milioni.
NEC kupitia ratiba hiyo iliyotolewa na Mkuu
wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura, Ruth Masham, ilionyesha mikoa mingi
nchini imepatiwa siku kati ya 28 na 30 kuandikisha wapigakura wakati katika
mikoa hiyo kukiwa hakuna mkoa unaozidi makadirio ya watu 1.5 milioni.
Dar es Salaam itaanza shughuli ya uandikisha
Julai 4 hadi Julai 16 mwaka huu wakati huo huo mikoa ya Arusha, Kilimanjaro,
Mara na Manyara iliyoanza Juni 12 nayo itakuwa ikiendelea kuandikisha hadi
Julai, 12.
NEC ambayo ilishapokea mashine zote za BVR
8,000, itakuwa ikiendelea kuandikisha mikoa ya Morogoro, Pwani na Tanga
itakayoanza Juni 18 hadi Julai, 18 siku mbili baada ya Dar es Salaam kumaliza
uandikishaji kwa mujibu wa ratiba hiyo.
0 comments:
Post a Comment