Hali hiyo ilijitokeza jana asubuhi katika
Kata ya Nshamba wilayani hapa wakati msafara wa Kinana ulipofika kuzindua mradi
wa maji. Kadhia hiyo ilianza baada ya Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera, Ally Idd
Ame kumkaribisha mbunge huyo ili awasalimie wananchi. Hata hivyo, wananchi hao
walianza kuzomea kwa zaidi ya sekunde 40 wakipinga Profesa Tibaijuka kupanda
jukwaani, hali iliyomlazimu Mkuu wa Wilaya, Francis Isack kupanda jukwaani na
kutoa kauli ya kiutawala ili kuwanyamazisha wananchi hao.
“Anayetaka kusikiliza abaki na asiyetaka
aondoke,” alisema Isack na kuwanyamazisha mamia ya wananchi hao. Baada ya kauli
hiyo wananchi walitulia na kuruhusu Profesa Tibaijuka kupanda na kuhutubia kwa
muda.
“Kama hamnitaki siyo lazima niwe mbunge wenu,
mnaruhusiwa kubadili. Huyo aliyewapa viroba asubuhi hii ili mje mnitie aibu
mbele ya katibu mkuu wa chama nawaambia hiyo dhambi itawatafuna,” alisema.
Aliwaambia wananchi hao kuwa anachokifanya ni
kuwatumikia na kuwaletea maendeleo, hasa wanawake...
“Mimi sitafuti kazi na wala sina njaa... na
kama hela ya kula ninayo. Mimi sigangi njaa na kama mnataka kuwa na kiongozi
mganga njaa muwekeni muone atawasaidia vipi,” alisema.
Akihitimisha salamu zake kwa wananchi hao
alisema kama wana jambo lao la ziada walifanye lakini wamuache aendelee na
jitihada za kuwaletea wanawake maji... “Sina kinyongo na yeyote kwa sababu “I
am too sophisticated (mstaarabu). Nipo juu ya mambo madogomadogo
yanayowasumbua.”
Mbunge huyo ambaye hivi karibuni aliondolewa
uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokana na kashfa ya Tegeta
Escrow, alimweleza Kinana kuwa eneo hilo limekumbwa na upinzani kutoka kwa mtu
anayehitaji kulichukua ambaye ni kutoka ndani ya CCM.
Profesa Tibaijuka alisema katika ubunge wake
amefufua mradi huo wa maji utakaogharimu Sh200 milioni kupitia shirika moja ambalo
mkandarasi wake ni wa Umoja wa Mataifa na utekelezaji umeanza miezi minne
iliyopita lakini unahujumiwa.
“Mradi huu wa Nshamba unahujumiwa na
wapinzani wangu kutoka ndani ya CCM na vyama rafiki vya kisiasa, lakini lengo
lao ni kunidhoofisha kisiasa, jambo ambalo linadidimiza maendeleo,” alisema
Profesa Tibaijuka ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Makazi la Umoja
wa Mataifa (UN – Habitat).
Kinana na kahawa
Katika ziara hiyo, Kinana aliitaka Serikali
mkoani Kagera kusimamia wakulima kuuza kahawa ndani na nje ya nchi ili
wanufaike badala ya kuwahusisha na magendo.
0 comments:
Post a Comment