Kufanyika kwa michezo hiyo iliyosimama miaka
mingi iliyopita baada ya Serikali ya Awamu ya Tatu, wakati ule chini ya Rais
Mstaafu Benjamin Mkapa, ambaye kupitia aliyekuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni,
Joseph Mungai iliisitisha kwa sababu ambazo zinadaiwa kuwa za michezo kuingilia
utoaji wa taaluma, ni jambo la faraja.
Tunasema, ni faraja kwetu kuona michezo hiyo
ambayo miaka ya 1970, 1980 na kidogo miaka ya 1990 ilikuwa yenye umuhimu mkubwa
na ambayo iliandaa na kisha kutoa wanamichezo wengi mahiri na ambao hatimaye
walikuwa wawakilishi wazuri kwa nchi yetu, inarejea wakati huu ambao michezo
imedorora na imepoteza mwelekeo.
Tunaipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi ambayo kwa kushirikiana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), wanaosimamia sekta ya elimu nchini kwa kuwezesha kufanyika
kwa michezo hiyo mjini Mwanza.
Hata hivyo, tukiwa wadau wa michezo,
tunapenda kutoa ushauri ambao ukizingatiwa, utaifanya Umisseta iwe yenye
manufaa na irejee kwenye msingi wa kuanzishwa kwake.
Kwanza, tunashauri michezo hiyo iwe ya
kitaifa kweli kama ilivyokuwa zama hizo ambazo ilifanyika kwenye kanda zote,
bara na visiwani na hivyo kusaidia kuimarisha Muungano kupitia michezo,
utamaduni.
Pili, tunashauri itumike kupata wanamichezo
bora ambao wataweza kusaidia nchi yetu kurejea katika ramani ya michezo kitaifa
na kimataifa, ambako imeporomoka kwa kiasi cha kutisha.
Tatu, tunashauri maadili yazingatiwe na
kupewa nafasi ya juu wakati wote wa michezo hiyo ili kuondoa kasoro ambazo
ziliibuka wakati wa michezo hiyo ikiwamo ya walimu na wakufunzi wa michezo hiyo
au wanafunzi wenyewe kuhusika kwenye vitendo viovu vikiwamo zinaa na
kusababisha mimba na magonjwa kwa baadhi ya wanafunzi.
Nne, tunashauri waandaaji wawe makini,
wazingatie nia na makusudio ya kufanyika kwake, kubwa likiwa ni kuwawezesha
wanafunzi kushiriki michezo na wataalamu wapate fursa ya kuchagua au kuteua
timu mbalimbali ambazo zitaiwakilisha nchi kitaifa na kimataifa.
Tunashauri kwamba ili kufikia azma hiyo,
lazima walimu wa michezo ambao wameandaliwa kwenye vyuo kama kile cha Malya,
wilayani Misungwi au Chuo cha Ualimu Butimba mjini Mwanza, ndiyo wapewe
jukumu la kuzinoa na kuziandaa timu hizo.
Tunaamini, vyama vya michezo na vingine vya
kitaaluma kama cha waamuzi, pia vitashirikishwa kwa karibu katika kuifanya
michezo hiyo iwe yenye heshima, staha na ambayo itatimiza malengo yake.
Tunaamini , vyama vya michezo kama TFF
(Shirikisho la Soka Tanzania) na vinginevyo vitashirikishwa katika maandalizi
ya michezo hiyo kila mwaka ambako watapatikana wanamichezo bora ambao
watasaidia kupata timu mbalimbali za kitaifa.
0 comments:
Post a Comment