Wakati huu ambao Watanzania wengi wanakumbana
na ugumu wa maisha, karibu kila kitu kimepanda bei, inaumiza kuona mijadala
ndani ya ukumbi wa Bunge ambao tuliambiwa miaka michache kwamba ulikuwa
umeigharimu nchi yetu kiasi kikubwa cha fedha, ambazo zinatokana na walipakodi,
ukumbi huo umegeuka kichekesho.
Ni kichekesho hiki, kwa sababu, kwanza hakuna
umakini kwa baadhi ya wajumbe wake, yaani wabunge wetu ambao wanaonekana kuwa
mjini Dodoma kimwili na wengine hawamo mjini humo, kwa sababu ambazo uongozi wa
taasisi hiyo unazitambua, naamini wabunge wapo mjini humo ili kutimiza
kile ambacho nasema hawakiamini hata kidogo.
Nasema hawakiamini, kwa sababu tunawaona
laivu kila siku kwenye runinga zetu wakibishana, wakati mwingine wakiwa kwenye
mambo madogo madogo ambayo yanasitikisha, mengi hayana tija.
Ni bahati mbaya, kama nilivyoeleza siku zote,
wakiwa Dodoma, wabunge ambao kwa sasa wamegeuza eneo hilo kuwa la kujinadi,
wengine wakipiga kampeni kana kwamba uchaguzi unafanyika kesho, utashangaa.
Baadhi yao, nasema wamejisahau,
unawaona wakipiga soga kwa kiasi kikubwa, hawasikilizi mijadala, hawachangii
hoja zilizoko mbele yao, kiasi kwamba ikifika wakati wa hotuba ya bajeti
utawasikia wakipingana nayo.
Kibaya zaidi, mipasho imegeuka kuwa sehemu ya
maisha ndani ya ukumbi huo wa Bunge ambao kwa kiasi kikubwa umepoteza hadhi ya
kuendelea kuitwa ‘kiota kitukufu’.
Ningekuwa na uwezo mimi, hakuna shaka
ningebali jina hilo la uheshimiwa, ambalo mmejiundia siku nyingi, lakini
hamliishi hata kidogo kama kweli waheshimiwa mbona mnaishi kwa kuparurana,
wakati mwingine kama watoto wa kijiweni?
Ninaamini, hata kama ni kampeni,
mtajirekebisha na kuacha masuala haya ya kitoto ambayo mnayafanya humo ndani ya
ukumbi wa Bunge.
0 comments:
Post a Comment