Hamasa na mapenzi makubwa waliyokuwa nayo
Watanzania kwa timu yao ya Taifa, Taifa Stars yamepotea siku za karibuni
kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo matokeo mabaya ya timu hiyo.
Hilo, limemfanya Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Said Mtanda afikirie kivingine na kutoa
ushauri.
Jana, Mtanda aliyekuwa mgeni rasmi kwenye
hafla ya uzinduzi wa jezi mpya za Stars alitaka mashabiki na wadau wengine wa
soka kurejesha mapenzi yao kwa Taifa Stars.
Uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam
ulikwenda sanjari na utoaji vyeti kwa makundi mbalimbali ya watu, waliotoa
mchango wao kwenye maendeleo ya mchezo wa soka nchini.
Katika uzinduzi huo, kulizunduliwa jezi aina
tatu, ambazo ni jezi za ugenini, jezi za nyumbani na jezi zitakazokuwa
zikitumika kwa ajili ya mazoezi.
Mtanda, ambaye ni Mbunge wa Mchinga mkoani
Lindi alisema uzinduzi wa jezi hizo uwe chachu ya kurudisha hamasa na mvuto wa
timu ya Taifa kwa Watanzania.
Alisema kuwa anaamini mabadiliko hayo ya jezi
yatakwenda sanjari na hatua madhubuti za kuziimarisha timu mbalimbali za Taifa
zifanye vizuri katika mashindano mbalimbali zitakayoshiriki.
“Kuna watu wanahoji hivi tunahitaji jezi mpya
au timu yetu ya Taifa kufanya vizuri? Mimi naona tunahitaji vyote viwili.
Tubadilishe namna ya kuendeleza timu yetu ya Taifa pia tubadilishe jezi
zinazotumiwa Taifa Star,” alisema Mtanda.
Jezi hizo zitaanza kutumiwa na Stars kwenye
maandalizi yao ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) na Michezo ya
wachezaji wa ndani (Chan), zitakuwa ni nyeupe kwa mechi za ugenini, wakati kwa
mechi za nyumbani zitakuwa za rangi ya bluu.
Akizungumza baada ya uzinduzi huo, kocha wa
Taifa Stars, Mart Nooij alisema kuwa kikosi chake kiko tayari kwa ajili ya
kupeperusha vyema bendera ya nchi katika mashindano yanayoikabili.
Nooij alisema kuwa kila mmoja kikosini
anatambua deni ambalo timu hiyo inalo kutoka kwa mamilioni ya Watanzania, hivyo
watapambana kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mechi hizo dhidi ya Misri
na Uganda.
“Tunaendelea na maandalizi yetu na molali ya
wachezaji iko juu. Wachezaji wanaendelea kuimarika siku hadi siku na kila mmoja
wetu anajituma kwa kadri ya uwezo na majukumu yake ili tuwape furaha
Watanzania,” alisema.
0 comments:
Post a Comment