Kama kuna jambo ambalo linatia doa mchakato mzima wa kuwapata
viongozi wa ngazi za juu katika nchi yetu, jambo hilo ni mifumo iliyopo
kufumbia macho umuhimu wa wagombea uongozi wa kisiasa katika ngazi hizo
kuonyesha rekodi yao ya ulipaji wa kodi za Serikali. Tofauti na mataifa
mengi duniani, Taifa letu limepuuzia suala la viongozi wake kuwa na
kiwango cha juu cha uadilifu na ufuataji wa maadili ya uongozi usioacha
shaka yoyote.
Moja ya masuala ambayo mataifa mengi ya nje
yametungia sheria kali na kuyaingiza katika katiba ni suala la ukwepaji
kodi. Ukwepaji kodi katika mataifa hayo ni kosa kubwa pengine kuliko
uhaini na yeyote anayetaka kuwa kiongozi anatakiwa kuonyesha rekodi ya
ulipaji kodi za serikali kwa kipindi kilichowekwa kisheria. Kiongozi,
hata akiwa mkuu wa nchi, akikutwa na hatia ya kukwepa kodi si tu
analazimika kujiuzulu nyadhifa zote alizonazo, bali pia anafungwa
gerezani.
Katika mataifa hayo, msemo kwamba ‘sheria ni
msumeno’ una maana kubwa, kwani sheria inatoa haki ama adhabu kwa tajiri
au maskini pasipo ubaguzi wa aina yoyote. Bahati mbaya hapa nchini,
mifumo ya kisheria na hata ya kikatiba imesukwa na kufinyangwa kwa namna
ambayo inawalinda matajiri na watu wenye madaraka na kuwafanya kuwa juu
ya sheria. Wanajiona ni raia wa daraja la kwanza na wananchi daraja la
pili. Mfano mdogo ni kifungu cha 39 (1) (e) cha Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kinachosema kwamba moja ya sifa za
mtu kugombea ubunge au urais wa nchi yetu ni iwapo katika kipindi cha
miaka mitano kabla ya tarehe ya uchaguzi mkuu atakuwa hajatiwa hatiani
katika mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kodi ya serikali.
Maana yake ni kwamba mtu yeyote ambaye alitiwa
hatiani na mahakama zaidi ya miaka mitano iliyopita kwa kukwepa kodi
(kiasi chochote) anaweza kugombea ubunge au urais kama anazo sifa
nyingine zilizoainishwa katika Katiba hiyo. Pengine yafaa tujiulize,
hivi mtu ambaye alihukumiwa kwenda jela kwa kukwepa kodi, kwa mfano,
atakuwa mbunge au rais wa namna gani na wananchi watamkubali vipi kama
kiongozi wao? Mtu huyo atakuwa hana ujasiri (moral authority) wa
kuwakosoa au kuwakemea wale anaowaongoza pale wanapokosea.
Ndio maana tunadhani kwamba wakati umefika wa
kuhakikisha mifumo ya kisheria na kikatiba inayowalinda viongozi
wasiwajibishwe inasukwa upya ili kuhakikisha inakuwapo mifumo
itakayoleta utawala bora na kusimika misingi ya maadili ya viongozi
katika serikali na taasisi za umma. Hapa nchini tungebadili mfumo wa
uteuzi wa viongozi, hasa wa ngazi za kitaifa kama urais na ubunge.
Wagombea katika ngazi hizo siyo tu waonyeshe rekodi zao za ulipaji kodi
katika kipindi kitakachowekwa kisheria, badala ya kuangalia tu kama
mgombea aliwahi kutiwa hatiani na mahakama kwa kukwepa kodi ndani ya
kipindi fulani.
Ukiwekwa utaratibu huo, hata utitiri wa wagombea
urais na ubunge tunaoshuhudia hivi sasa hautakuwapo. Kwa mfano, watiania
watakiwe kuonyesha kama wamekuwa wakilipa kodi ya ardhi, majengo,
viwanja, biashara, hisa na kodi nyingine. Zipo tuhuma kwamba viongozi
wengi nchini hawalipi kodi hizo na wamekuwa kikwazo kwa taasisi
zinazokusanya kodi.
0 comments:
Post a Comment