Baadhi yao walichukua fomu hizo, baada ya
kwanza kuandaa mikutano mikubwa katika kumbi mbalimbali au viwanja vya mpira,
na kutangaza nia huku wengine wakichukua kimyakimya bila ya kujinadi japo
baadaye walizungumza na vyombo vya habari. Orodha ya waliochukua fomu kupitia
CCM ni ndefu na ni jambo lenye afya katika demokrasia.
Tunawapongeza wagombea wote. Masikitiko yetu;
kwanza, ni kuona baadhi ya wagombea hao wakiwabeza wenzao, kuonyesha kwamba
hawana uwezo, hakuna anayefaa kuliko wao. Pili, ni kauli zao za kuiponda hata
Serikali hii ya awamu ya nne iliyoundwa na chama chao.
Tatu, ni ahadi nyingi zinazotolewa na
wagombea hao juu ya mambo watakayotekeleza ikiwa watateuliwa kugombea na
kushinda urais katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Tunawatahadharisha wananchi wawe macho.
Mfano, baadhi ya wagombea wamedai watajenga reli kuunganisha mikoa, kujenga
viwanda ili uchumi wa nchi uendeshwe na viwanda, kupambana na mafisadi
waliolelewa na kukingiwa kifua na serikali, kuendesha nchi bila kutegemea hata
senti kutoka nchi wahisani na kuteua baraza dogo la mawaziri.
Wengine wamedai watarejesha Azimio la Arusha,
kila nyumba itakuwa na mabomba mawili; moja la kuingiza maji na jingine
kuingiza gesi, kuifikisha nchi kuwa ya uchumi wa kati, kuigeuza Tanzania kuwa
nchi mpya – nchi ya asali na maziwa, na kutekeleza yaliyomo kwenye Ilani ya
Uchaguzi ya CCM.
Ahadi hizo – wananchi wasipojiuliza swali
watatekeleza vipi – ni tamu masikioni na ndiyo maana kila mtangazania
alishangiliwa sana na umati mkubwa wa wafuasi wake waliofurika kumsikiliza,
wakiwamo baadhi ya viongozi mashuhuri wastaafu. Hata hivyo, baadhi ya wananchi
wamekuwa wakiwashangilia watangazania kwa vile wanatoka maeneo yao lakini si
uhalisia wa ahadi.
Hebu wananchi jiulizeni, ikiwa kwa miaka 54
ya uhuru, watu wanahangaika na maji na wakipatiwa ni ya visima, ni miujiza gani
itafanyika kwa miaka mitano kila nyumba, hata za mbavu za mbwa, kuwa na mabomba
ya maji na gesi? Vipi watajenga viwanda vipya wakati sera ya Serikali ni
kutokujihusisha na biashara?
Baadhi ya wagombea hao wamezeekea katika
utumishi serikalini, wameshuhudia na kuhusika kukingia kifua mafisadi, leo
wanaposema watapambana na wala rushwa, watafanya miujiza gani kuondoa kansa
hiyo?
Jiulizeni, kati ya watangaza nia hao, ni nani
amethubutu bungeni kupigia kelele ufisadi kupitia ununuzi wa rada, Richmond na
Escrow? Ni wizara gani haijawahi kukumbwa na dosari za udhibiti wa fedha kama
inavyoainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali? Watu walifikia
kuiba hata fedha za safari wakidai ni za safari za rais wakati ni uongo!
Kwanini baadhi yao walifukuzwa uwaziri?
Hatuna nia ya kuwapinga wagombea hao, lakini
wawe wakweli, ahadi walizotoa nyingi hazitekelezeki. Hata Serikali ya Awamu ya
Nne iliingia madarakani na ahadi nyingi tamu kwenye masikio ya wapigakura,
lakini hadi leo kila eneo wanalalamika ahadi ya rais haijatekelezwa na sababu
kubwa hazikuwamo kwenye Ilani ya Uchaguzi. Hivyo, tunawatahadharisha wananchi
kwamba wote wanaoshangilia ahadi ambazo hazimo kwenye ilani watachagua rais
kanyaboya.
0 comments:
Post a Comment