KOCHA wa Yanga, Hans van der Pluijm amevutiwa na viwango vya
wachezaji wake wapya katika kikosi hicho kwa kile alichokisema kuwa wote
wamefanya vizuri katika mchezo wa juzi.
Katika mchezo huo wa kirafiki uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa
kati ya Yanga dhidi ya Sports Club Villa ya Uganda, timu hizo zilitoka
suluhu.
Wachezaji wapya wa Yanga waliocheza kikosi cha kwanza ni Deus Kaseke,
Malimi Busungu na Godfrey Mwashiuya, ambao kwa mujibu wa Pluijm,
walicheza vizuri kwa kujituma.
“Wachezaji wote wamejitahidi wamecheza vizuri, wameshirikiana vizuri
katika kikosi hicho,” alisema. Licha ya kuwa mchezo huo ulikuwa ni kwa
ajili ya kuwachangia walemavu wa ngozi (maalbino) ulitumika pia kuwapima
wachezaji hao wapya kwa kuwaonesha mashabiki viwango vyao.
Wachezaji hao kila walipokuwa wakigusa mpira na kucheza vizuri
walikuwa wakipigiwa makofi na mashabiki wa klabu hiyo waliohudhuria kwa
wingi huku wengine wakionekana kuvutiwa na viwango vyao kutokana sifa
walizokuwa wakizitoa wakati mechi inaendelea.
Pluijm alizungumzia pia kuhusu kiwango cha timu na kusema licha ya
kucheza vizuri walitamani kupata ushindi. “Kikosi kilicheza vizuri,
tulitengeneza nafasi za kufunga lakini bahati haikuwa ya kwetu, wenzetu
walianza vizuri lakini baadaye wakajikuta wanacheza kwa kuzuia,”
alisema.
Alisema mchezo huo umempa nafasi ya kujua baadhi ya mapungufu, hivyo
atayafanyia kazi na kujipanga kwa ajili ya michezo mingine ijayo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment