WACHEZAJI wawili na makocha wawili wa timu ya Mwadui ya Shinyanga
wamenusurika kifo baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali
mkoani Dodoma.
Wachezaji hao ni kiungo wa zamani na kipa wa zamani wa Yanga, Nizar
Khalfan na Shaaban Kado. Kado, ambaye amejiunga na Mwadui akitokea
Coastal Union, ameumia vibaya mkono wa kulia katika kiwiko.
Walipata ajali hiyo jana saa saba mchana eneo la Bahi mkoani Dodoma
wakienda Shinyanga kuendelea na mazoezi waliyoanza jijini Dar es Salaam
kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoanza Agosti.
Makocha wao, kocha msaidizi Habib Kondo na yule wa makipa
aliyetambuliwa kwa jina la Adam Khalid, wamepata michubuko. “Tunashukuru
tuko salama, ajali hii ni mbaya, tungeweza hata kugonga basi lililokuwa
mbele yetu,” alisema Khalid.
Katika basi hilo kulikuwa na wachezaji wengine takribani 10
wakiongozwa na Julius Mrope. Hata hivyo, gari lao aina ya Toyota Grandis
limeharibika vibaya hasa nyuma baada ya kupasuka matairi ya kulia na
kuchomoka.
Kado na Nizar waliondoka kwa basi la Isamilo Express kuendelea na
safari wakiungana na wenzao waliopanda basi hilo kuanzia Dar es Salaam.
Mwadui FC iliyopanda Ligi Kuu msimu ujao, inaanza maandalizi ya ligi
inayoanza Agosti 22, mwaka huu.
Wengine ni Malika Ndeule, Said Sued, Jabir Aziz na wengineo. Gari
hilo lilikuwa likiendeshwa na Kondo, beki wa zamani wa klabu kadhaa
nchini.
Gari hilo lina namba za usajili T444 DCX. Wachezaji hao walipewa
huduma ya kwanza eneo la ajali na kisha polisi kuandika maelezo yao.
Mwadui inafundishwa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye inaelezwa
alitumia usafiri wa ndege jana kwenda Shinyanga. Akizungumza kwa njia ya
simu jana, Kihwelo alikiri kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa Kado
aliumia kidogo kiwiko cha mkono na waliruhusiwa kuondoka kuenda
Shinyanga.
Alisema kuwa timu hiyo ilikuwa ikienda Shinyanga kuendelea na mazoezi yaliyoanza jijini Dar es Salaam wiki moja iliyopita.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment