HUKU ikishuhudiwa na wachezaji wake wa kigeni Donaldo Ngoma na Joseph
Tetteh Zutah waliowasili Dar es Salaam jana, Yanga ilijikuta ikitoka
sare ya bila kufungana na Sports Club Villa ya Uganda kwenye mchezo wa
kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwenye mechi hiyo maalumu kwa ajili ya kupinga mauji ya albino na
mgeni rasmi kuwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Mecky Sadiki,
Yanga ilipoteza nafasi nyingi za kufunga kwenye mchezo huo.
Washambuliaji wa Yanga wakiongozwa na Amisi Tambwe na Simon Msuva
walishindwa kufurukuta mbele ya ukuta thabiti wa Sports Club Villa ambao
ni mabingwa wa Uganda.
Yanga iliwachezesha wachezaji wake wapya iliowasajili msimu huu kama
vile winga Deus Kaseke aliyetoka Mbeya City, Malimi Busungu aliyetoka
Mgambo JKT na chipukizi Godfrey Mwashuiya aliyesajiliwa wakati wa
dirisha dogo walishindwa kabisa kuipenya na kushuhudia wakipoteza nafasi
kadhaa za kufunga hasa kipindi cha kwanza.
Malimi Busungu alikosa bao la wazi kwenye dakika ya 31 baada ya
kupokea pasi nzuri ya winga Goefrey Mwashuiya, lakini mpira aliopiga
ulitoka pembeni kidogo ya Yanga la Sports Club Villa na dakika ya 39
Amis Tambwe alikosa bao la wazi akiwa ambeki peke yake na kipa wa Villa
Sebweto Nicholaus.
Kwenye mchezo huo, kiungo Lasana Kamara kutoka Mali, aliyekuwa
akifanya majaribio na Yanga aliibukia SC Villa na kuonyesha kiwango
kizuri.
Kwenye mechi hiyo timu zote zilifanya mabadiliko kadhaa kwa Yanga
kuwapumzisha Malimi Busungu na kumuingiza Kpah Sherman na Nadir
Haroub’Cannavaro’ alitoka baada ya kuumia na kuingia Pato Ngonyani.
Huku Villa ikiwatoa Kasule Abdulkarim na kumuingiza Dua Abeid na kisha kumtoa Kazibente James na kumuingiza Kamazi Dennis.
Hata hivyo Yanga walipata penalti kwenye dakika ya 79 baada ya Deus
Kaseke kuangushwa kwenye eneo la hatari lakini Simon Msuva alipaisha
penalti hiyo na kuinyima Yanga ushindi kwenye mechi hiyo ya kujipima
nguvu kujiandaa na mashindano ya kombe la Kagame.
Yanga mpaka sasa imecheza michezo miwili ya kujipima nguvu ambapo
wiki hii iliifunga klabu ya daraja la kwanza ya Friends Rangers kwa
mabao 3-2 kwenye mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment