Tambarare Halisi jana tuliandika habari iliyosema wabunge 33 ndiyo waliopitisha Muswada wa Benki ya Posta
Tanzania. Idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya wabunge wote
ambao ni 356 na nusu yao ni 178. Mahudhurio duni bungeni yameanza
kukithiri katika Bunge hili la 10 na kuzoeleka kama tabia au utamaduni
mpya wa wabunge.
Hali hii ilimkera hata Spika wa Bunge, Anne
Makinda ambaye aliikemea tabia ya utoro kwa wabunge akisema kuwa baadhi
yao wamekuwa na tabia ya kukacha vikao na kusafiri bila ruhusa yake wala
ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Tunaungana na Spika Makinda kukemea utoro, lakini
pia tukishangaa yanayoendelea bungeni ikiwamo wabunge kiduchu kupitisha
miswada mbalimbali ya Serikali na hata bajeti za wizara.
Kuna mifano mingi kuhusiana na hilo. Wakati wa
kupitisha Muswada wa Sheria ya Masoko ya Bidhaa wa mwaka 2015,
mahudhurio yalikuwa duni kwani ni wabunge 37 tu ndiyo walipitisha
muswada huo huku mawaziri na naibu mawaziri wakiwa wanne tu.
Pia, mjadala wa muswada wa Sheria ya Usimamizi wa
Maafa ulihudhuriwa na wabunge 81, lakini hali ilikuja kuwa mbaya zaidi
wakati wa kujadili Muswada wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Silaha
na Risasi, ambako kulikuwa na wabunge 29.
Hata hivyo, hoja za baadhi ya viongozi
wanaosimamia vikao vya Bunge zimeonekana kuitetea hali hiyo. Mathalan,
Naibu Spika Job Ndugai alinukuliwa na gazeti hili akisema akidi hupimwa
kwa jicho la Spika na kwa uthibitisho wa macho yake, Bunge lilipitisha
Muswada wa Benki ya Posta Tanzania, huku idadi ya wabunge ikiwa ni 33
tu.
Mtetezi mwingine ni Mwenyekiti wa Bunge, Mussa
Azzan Zungu ambaye amewahi kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari,
akitetea kuwa bajeti za wizara zinaweza kupitishwa hata kama idadi ya
wabunge ikiwa ndogo, isipokuwa kwa bajeti kuu kwamba hapo lazima akidi
izingatiwe.
Lakini jambo la ajabu katika kikao hiki hiki,
Naibu Spika Ndugai alilazimika kuahirisha kupitishwa kwa bajeti ya
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, baada ya kujiridhisha kuwa idadi
ya wabunge waliokuwapo ukumbini wakati huo ilikuwa ndogo, hadi
anaahirisha kikao, ukimbini kulikuwa na wabunge 110.
Ndugai aliahirisha kikao baada ya Mbunge wa
Kuteuliwa, James Mbatia kutumia Kifungu namba 112 (1) cha Masharti ya
Kanuni ya 77 kinachosema kwamba, Kamati ya Bunge zima haitafanyika pale
idadi ya wabunge waliohudhuria itakapokuwa bado haifikii nusu ya wabunge
wote.
Zungu anasema bajeti za wizara zinaweza kupitishwa
hata kama akidi haitimii, Naibu Spika Ndugai anasema akidi inapimwa kwa
macho, lakini anapochachamaliwa na wabunge anakubali kufuata kanuni
kuhusiana na akidi. Tunahoji kwa nini Ndugai awe na kauli mbili tofauti?
Ukiisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Ibara ya 94 (1) inaeleza kuwa upitishwaji wa jambo lolote
linalohusu uamuzi wa wabunge, ni lazima akidi iwe ni nusu ya wabunge
wote kama ilivyo Kanuni ya 77 ya Bunge.
Tungependa kuwakumbusha wabunge wetu kwamba akidi
katika mijadala na wakati wa kupitisha miswada na bajeti za wizara
mbalimbali ni jambo muhimu, pia kanuni na sheria kuhusu akidi zifuatwe.
Wabunge wachache kufanya uamuzi wa Bunge ni jambo ambalo halikubaliki na
ni sawa na kuwakejeli wananchi waliochagua.
0 comments:
Post a Comment