Tukio la
kutwangana makonde lilitokea katika Kituo cha Shule ya Mwangaza,Gongo
la Mboto saa 2.15 asubuhi wakati uandikishaji ulipokuwa ukianza.
Mashuhuda
wa tukio hilo walisema: “Polisi unaowaona wamefika muda si mrefu, wala
hawakuwepo hapa tangu asubuhi... ninadhani walipewa taarifa baada ya
watu kuanza fujo wakigombania kuingia ndani kujiandikisha,” alisema
Magreth John na kuongeza:
“Watu wamepigana kwa sababu
wanasema kuna wenzao ambao majina yao hayakuandikwa jana (juzi) halafu
wamefika asubuhi wakaanza kuitwa ndani kujiandikisha. Hapo ndipo mzozo
ulipoanzisha na ngumi zikafumuka.”
Msimamizi wa kituo hicho, Ramadhani Mshindo alisema mzozo huo ulitokea kwa sababu ya wananchi hao hawakuelewa utaratibu.
“Jana
(juzi) jioni wakati tunafunga zoezi hili saa 12.00 jioni kuna watu
wengi walikuwa kwenye foleni ambao hawakuandikishwa, kwa hiyo
tuliwaandika majina ili leo (jana) wakifika hapa watangulie kuandikishwa
kabla ya wengine. Sasa tulivyofika na kuanza kuita majina yao ili
waingie kujiandikisha ndipo watu wakaanza fujo na kupigana ikabidi
tupige simu polisi ili waje kutuliza ghasia,” alisema Mshindo.
Katika
Kituo cha Shule ya Msingi Jica,Tabata wananchi walilalamikia suala la
muda kwani waandikishaji walichelewa na hadi saa 4.30 asubuhi, asilimia
kubwa ya watu hawakuwa wamepata huduma. “Nimefika hapa saa 12.00 asubuhi
lakini hadi sasa sioni dalili ya kuandikishwa leo… Wametuambia wanaanza
kuandikisha wale waliobaki jana kwa sababu majina yao yaliandikwa kwa
hiyo sisi wa leo tunasubiri kwanza,” alisema Maria Saleh.
Maria alisema uandikishaji unakwenda taratibu kutoka na mashine kugoma mara kwa mara.
Malalamiko
kama hayo yalitolewa na wananchi waliokuwa wamefika kujiandikisha
katika Kituo cha Shule ya Msingi, Ulongoni,Gongo la Mboto na waandishi
wetu walishuhudia watu wengi wakiwa kwenye misururu, wengine wakiwa
wamelala pembeni ya kituo hicho baada ya kuchoka kusimama muda mrefu.
Hata
hivyo, kwenye kituo hicho, wananchi walijiwekea utaratibu kwamba kila
mtu anayefika anaandika namba kwenye daftari na kupewa kikaratasi kidogo
chenye namba hiyo ndipo anapanga foleni.
Utaratibu ambao ulisaidia kupunguza usumbufu na kuondoa vuta ni kuvute wakati wa kuingia kwenye chumba cha kujiandikisha.
Lakini licha ya kujiweka utaratibu huo, Ibrahim Kitumbi alisema changamoto ya muda na vifaa ilikuwa palepale.
“Hivi
tunavyozungumza watu waliyopewa namba wamefika 2,145. Hawa wameandika
majina tu na kupewa namba. Waliojiandikisha tangu jana hawafiki hata
200. Sasa kwa siku nane zilizobaki kweli tunaweza kumaliza kuandikishwa!
Huku si kutunyima haki?” alihoji.
Wakati wananchi
wakitoa malalamiko hayo, Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Ulongoni, Majura
Mtalemwa alisema zoezi la uandikishaji linakwenda vizuri tofauti na
wananchi wanavyolilalamikia.
Mkazi wa Temeke, Steven
Almasi aliyefika kujiandikisha katika Kituo cha Magogoni, Yombo alisema
mwaka huu wa uchaguzi kuna uwezekano mkubwa wa baadhi ya wananchi
kutoshiriki uchaguzi.
Mtendaji wa mtaa huo, Zeddy Zeddy alikiri kuwapo baadhi changamoto kwenye kituo chake ikiwamo uchache wa mashine za kuandikisha.
“Mwitiko
wa watu umekuwa mkubwa tofauti na matarajio yetu kwa hiyo kama mashine
zikiongezwa kwenye baadhi ya vituo, itasaidia kuondoa msongamano na kazi
kukamilika kwa wakati,” alisema Zeddy.
“Kama Tume
ingeongeza mashine,mambo yangekwenda vizuri zaidi lakini kinachoendelea
ni ngumu kusema kuwa watu wote wataandikishwa kama ilivyopangwa,”
alisema mtaalamu wa BVR aliyekuwapo Kituo cha Shule ya Msingi Kibangu,
Ubungo, Suleiman Mahmoud.
Katika kituo cha Kontena –
Tanesco, Kinondoni ni mashine moja tu iliyokuwa ikifanya kazi kati ya
tatu kutokana na kuharibika licha ya idadi ya watu kuwa wachache.
“Mashine
moja ilikuwa haifanyi kazi hadi saa tatu asubuhi, wameleta nyingine
lakini nayo kamera inasumbua. Hii yangu printa haifanyi kazi hivyo ipo
moja tu. Tumewapigia IT (mafundi wa Teknolojia ya Mawasiliano) wamesema
wanakuja lakini wengi wanatembea kwa miguu wanachelewa kufika,” alisema
mwendeshaji mashine ya BVR kituoni hapo, Max Phillipo.
Mkazi
wa Mwananyamala, Hemed Shefaya alisema alifika kituoni tangu saa 10
alfajiri akiwa na wenzake watatu lakini kilifunguliwa saa 2.30 asubuhi.
“Mashine
hizi zinaharibika mara kwa mara, kwa sasa wamezitengeneza lakini mikono
ya wasimamizi ni mizito sana. Tulikuja jana na kupatiwa namba lakini
hatukufanikiwa kuandikishwa… fikiria mimi namba 18 ya jana nimekuja saa
12 asubuhi lakini bado hadi sasa (saa 5.43) sijaandikishwa,” alisema
Ramadhani Mkombozi aliyekuwa katika Kituo cha Shule ya Msingi Kisiwani,
Mwananyamala.
Ofisa Uchaguzi wa Manispaa ya Kinondoni,
Valence Urassa alisema tatizo la kuharibika kwa BVR lilikuwa likifanyiwa
kazi na mafundi wa NEC na Manispaa na kwamba maeneo yenye wakazi wengi
yalikuwa yakiongezwa mashine kufikia mbili kila kituo.
Kuhusu
kuchelewesha kufungua vituo, alisema kituo chochote hakitafunguliwa
2.00 asubuhi iwapo waandikishaji hawatakuwa wamekamilisha maandalizi ya
vifaa na kuandikisha kwani kuwahisha kutaleta matatizo.
Baadhi ya wasimamizi wametoa wito kwa NEC kuongeza vifaa pamoja na wataalamu ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati.
Msimamizi
wa Kituo cha Chuo cha Usafirishaji (NIT), Kelvin Donald alisema mashine
alizonazo zinasumbua tangu juzi na hata baada ya kutoa taarifa na
kubadilishiwa bado tatizo hilo linaendelea.
“Kwa wastani wanajitokeza watu 1,200 kila siku na hapa tuna mashine tano tu, moja haifanyi kazi,” alisema Donald.
Mwenyekiti
wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi Luis, Omari Mshauri alisema baada ya umeme
kuwa kikwazo, juzi msamaria mmoja alijitolea jenereta huku wengine
wakichangia mafuta kuendelea na kazi.
NEC yafafanua
Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa NEC, Julius Malaba alisema wakazi wote wa jiji hili
waliojitokeza wataandikishwa hata baada ya siku zilizopangwa kumalizika
hivyo hawatakiwi kuwa na hofu.
“Hakuna mtu aliyejitokeza kuandikishwa halafu akaachwa… tutaandikisha mpaka wote waliojitokeza siku ya mwisho watakapokamilika.
“Mpaka
sasa tuna mashine takriban 3,500 na nyingine zinaendelea kuingia kutoka
mikoa ambayo tumeshakamilisha kuandikisha. Hizi zote zitaletwa kuongeza
nguvu ya uandikishaji katika maeneo yenye wakazi wengi na kumaliza
haraka,” alisema Malaba.
Kawe kujiandikisha upya
Malaba
alieleza kuwa wakazi wa Jimbo la Kawe ambao walijiandikisha awali
katika uandikishaji wa majaribio, watatakiwa kujiandikisha upya ili
wapate vitambulisho vya sasa.
Hata hivyo, hakutaja sababu za kurudia na kuahidi kufafanua zaidi leo.
RC atoa maagizo
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik amewataka wakurugenzi wote wa
Manispaa za Dar es Salaam kutoka maofisini na kwenda kusimamia kwa
karibu uandikishaji huo na kutatua matatizo yanayoripotiwa na wananchi
kila wakati.
Alisema amepokea malalamiko mengi kutoka
kwa wananchi, mojawapo likiwa waandikishaji kuchelewa kufika vituoni,
kuwahi kuondoka kabla ya muda na mashine kugoma.
“Tutachukua
hatua kali kwa ofisa mwandikishaji yeyote atakayekiuka taratibu na
kukwamisha uandikishaji... tunafahamu uandikishaji unakabiliwa na
changamoto nyingi, lakini nimepata taarifa kuwa waandikishaji pia
wanahujumu uandikishaji bila sababu za msingi,” alisema Sadik.
Kwamsuguli.
Kwamsuguli.
Changamoto bado inaonesha kuendelea kuwa kubwa katika vituo
mbalimbali vya uandikishaji wananchi kwenye daftari la wapiga kura katika ofisi
ya mtaa temboni eneo la kwamsuguli temboni jijini Dar es Salaam,ambapo hali ya
foleni imeonekana kuwa kubwa huku wananchi wakiwa wamepanga mistari huku
wengine wakionekana kukata (tamaa)na kukaa chini kwa kutojua sangapi
wanaandikishwa.
Mwananchi aliyetupasha taarifa hii amesema watu walioanza
kuandikishwa ni wachache huku wengine hata kupata tu namba ni shida hivyo
nivyema mamlaka husika iangalie kwa kina zoezi hili ni namna gani ya kuweza
kufanya ili watu wote waweze kuandikishwa.
Makangarawe.
BVR-Kwenye wilaya ya Temeke,Tarafa ya Makangarawe kwenye kituo cha uandikishaji wanachi kwenye
daftari la wapiga kura Katika Kituo cha BUZZA Kanisani shule napo hali si shwari
kwani zoezi linaelezwa linasuasua kwa
hivyo kuchukua muda mwingi huku watu
wakiwa ni wengi,wanaomba utatuzi kwa mamlaka husika.
0 comments:
Post a Comment