Zoezi la uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa
teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR) katika Jiji la Dar es
Salaam, limekuwa mshikemshike ingawa awali Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), iliweka bayana kwamba litakuwa jepesi kwa kuwa mashine zote
8,000 zingetua Dar.
Zoezi hilo ambalo lilianza Julai 22 na kutazamiwa kuhitimishwa Julai 31,
mwaka huu kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck
Sadiki, kila kukicha limekuwa likikumbwa na sarakasi, vituko na majanga
kutokana na kutokuwepo usimamizi mzuri katika uandikishaji.
RC Sadiki awali kabla ya uandikishaji alisema kuwa takriban wakazi
milioni mbili wanatarajiwa kuandikishwa katika BVR na kwa wakazi wenye
sifa takriban milioni mbili wa jiji la Dar es Salaam.
Akaongeza kuwa vituo 1,684 vitatumika katika uandikishaji ambapo katika
manispaa ya Ilala vituo 396, Temeke 572 na Kinondoni 706.
Kwa upande wa Manispaa ya Temeke watakuwepo maofisa waandikishaji 1,144
ambapo wa akiba ni 128, waandishi wasaidizi 572 na na wa akiba 128.
Manispaa ya Ilala maofisa waandikishaji watakuwa 792 na wa akiba 144, waandishi wasaidizi 136 na wa akiba 144.
Aidha, Sadiki akasema katika manispaa hizo kutakuwepo na ofisa
mwandikishaji wa Halmashauri, Ofisa uchaguzi, maofisa wasaidizi wa
majimbo na kata na wataalamu wa Tehama.
Ukiangalia tarakimu hizi, utajiridhisha kwamba endapo uratibu na
usimamizi utakuwa mzuri, hayatakuwepo malalamiko yoyote katika zoezi
zima.
Lakini cha ajabu ni kwamba viongozi wetu wanageuka kuwa wazungumzaji
wazuri wa mipango ya kuwahudumia wananchi lakini kumbe ni kiini macho
tu.
Uandikishaji Dar hadi sasa umekuwa ni kero, malalamiko, misururu ya
foleni inayochefua, jambo ambalo pia limechangiwa na baadhi ya viongozi
na watendaji kutumia mwanya huo kujinufaisha.
Wengine bila hata aibu wameanzisha mradi kwa kuandikia watu vimemo
ambavyo hupita navyo milango ya nyuma ili waandikishwe haraka, kisa tu
katoa rushwa kwa mtendaji na washirika wake.
Mtu anaandikiwa leo kikaratasi na mtendaji kikimwelekeza kuja kituoni
kesho yake kwa ajili ya kujiandikisha. Afikapo anahudumiwa haraka kwa
kuwa tayari alishatoa rushwa.
Wananchi wengi wameitikia wito wa kuandikishwa lakini wanakatishwa tamaa
jinsi zoezi linavyofanyika, huku wengine wakilala vituoni ili kuwahi
nafasi. Mara zitolewe namba ambazo wengine wanabaki nazo mikononi wakati
wengine wanaopenyezwa kwa vimemo wanahudumiwa na kuondoka haraka.
Hii ni aibu na dhambi kubwa kwa viongozi wetu ambao wanavuruga taratibu pasipo sababu ya msingi.
Wananchi wanategemea kuwa haki inatendeka kwa yule aliyewahi kituoni
kuhudumiwa kwanza na siyo aliyekuja mwisho, kwa sababu tu ametoa rushwa.
Siyo hivyo tu, katika maeneo mengine hata hao maofisa uchaguzi na
wasaidizi wa majimbo na kata hawaonekani ili kuweza kusimamia
kuhakikisha uandikishaji unakwenda inavyotakiwa.
Pia limezuka tatizo la baadhi ya mashine za uandikishaji kufichwa kwenye
nyumba za watu. Hii ikitia shaka kuwa huenda lipo zoezi la siri
linalofanyika kuandikisha watu kinyemela kwa sababu zisizofahamika. Hii
ni dhambi ambayo ina mwisho wake.
Sisi tulidhani kuwa kwa sababu mashine zote zilizokuwa zikitumika nchini zitamwagwa Dar, basi uandikishaji hautakuwa na tatizo.
Na katika vituo zingekuwepo mashine zaidi ya moja ili kuharakisha zoezi,
hasa kwa kuzingatia kwamba muda wa siku kumi uliotolewa unaweza
usitoshe kwa kila mlengwa kuandikishwa.
Viongozi wetu ni muhimu wawe makini linapofanyika jambo la kitaifa kama
hili la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura. Wasiwe watu wa
maneno tu pasipo vitendo. Kama umepangiwa kusimamia eneo fulani, timiza
wajibu wako.
Lakini pia viongozi wa ngazi za juu kwenye tume ni muhimu waweke mfumo
wa ufuatiliaji wa karibu kuona kwamba maofisa wake pamoja na wasaidizi
hao wanasimamia yale waliyoelekezwa na siyo kuishia kupeana posho lakini
maeneo ya usimamizi hawapo.
Na hicho ndicho kilichojitokeza Dar es Salaam kwa sababu katika vituo
vingi, maofisa wa ufuatiliaji hawapo na ndio maana malalamiko yamezidi
kuwa mengi kiasi cha wengine kukata tamaa ya kujiandikisha.
Tume ya uchaguzi ijipange isifanye masihara na masuala kama haya ya
kitaifa. Tunajiuliza; Huu ni uandikishaji tu, ikifika uchaguzi
itakuwaje?
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment