Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa kikao
kirefu cha majadilino cha viongozi wa vyama vinavyounda umoja huo jijini
Dar es Salaam jana usiku, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia,
alisema wamekubaliana kutangaza mgombea baada ya siku saba li kutoa
nafasi kwa viongozi walioshiriki majadaliano hayo kutoa taarifa kwa
wanachama wa vyama vyao juu ya mambo waliokubaliana.
Ukawa unaundwa na Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi na NLD.
Viongozi hao kwa siku nzima ya jana walijifungia ili kusaka
muafaka ikiwa ni muendelezo wa vikao kadhaa kama hivyo juu ya mgawanyo
wa majimbo na mtu anayefaa kusimamishwa kugombea urais.
Aidha, Mbatia alikanusha uvumi kuwa kada wa CCM Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa, ana mpango wa kujiunga na umoja huo ili apewe
nafasi ya kugombea urais baada ya kukosa nafasi hiyo kupitia chama
chake.
“Huo ni uvumi tu wa kwenye mitandao na hata sisi tunashangaa
taarifa hizo zinatoka wapi. Sisi tumeshamaliza mchakato wetu wa kumpata
mgombea wa urais na tutamtangaza rasmi baada ya siku saba kuanzia sasa,”
alisema.
Mbatia pia alikanusha uvumi ulioenea kwenye mitandao ya kijamii
kuwa kuna mvutano mkubwa ndani ya Ukawa katika suala la mgombea urais
ambao umesababisha CUF kutaka kujitoa.
“Hakuna ukweli katika hilo na hata leo (jana) nimeongea na Prof.
Lipumba (Prof. Ibrahimu Lipumba, Mwenyekiti wa CUF) kumtaarifu hatua
tulioyofikia hivyo hakuna mpasuko wowote,” alisema Mbatia.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya kikao hicho cha viongozi wa juu
wa vyama vinavyounda Ukawa zinasema kuwa viongozi wakuu wa CUF,
Mwenyekiti Lipumba na Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad au
Naibu wake, Magdalena Sakaya, hawakuhudhuria. Waliwakilishwa na kiongozi
mmoja mwandamizi.
Vyama vingine, walihudhuria wenyeviti na makatibu wao.
Jana Watanzania walikuwa na matarajio kuwa mgombea wa Ukawa
angetangazwa, hata hivyo baada ya kusubiri kwa muda mrefu, taarifa
iliyotolewa usiku imesogeza tena mbele muda wa kumfahamu kwa siku saba.
Awali Ofisa wa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, aliwaambia waandishi wa habari kuwa:
"Mambo mengine yote yameisha, sababu iliyofanya majadiliano kuwa
marefu na kuchelewa kutolewa kwa taarifa hadi sasa ni majimbo mapya
yaliyoongezwa na kutangazwa na Nec, "alisema.
Ijumaa iliyopita Ukawa walitoa taarifa ya kwamba wangemtangaza mgombea wake ndani ya saa 24, ahadi ambayo haikutimizwa.
0 comments:
Post a Comment