Image
Image

Lembeli akataa kubadili msimamo.

Mbunge wa Kahama aliyemaliza muda wake, James Lembeli amekataa kubadili msimamo wake wa kutogombea ubunge kupitia CCM akisema atagombea nafasi hiyo kupitia chama kingine.
Akizungumza mjini hapa jana, Lembeli alisema hawezi kubadili msimamo wake wa kuondoka CCM, kutokana na masharti mazito ya kimila aliyopewa kabla ya kutangaza kuondoka katika chama hicho.
Baada ya uamuzi wake, watu mbalimbali, wakiwamo maofisa wa Serikali na wafanyabiashara waliahidi kumsaidia hata nguvu ya kifedha, wakimtaka atengue uamuzi wake achukue fomu katika Jimbo la Kahama Mjini.
Alisema hawezi kukiuka masharti ya kimila kwa kuwa yeye ni mtoto wa chifu. Mtoto huyo wa Chifu Daud Lembeli alisema kabla ya kutoa uamuzi huo alikaa na mama yake mzazi, Maria Kalembo kuanzia saa 10 jioni hadi saa nane usiku akizungumzia suala hilo hadi walipokubaliana.
Alisema baada ya mama yake kukubali na kutoa baraka za kuhama CCM, alipigiwa ngoma za kimila za Waswezi, ambazo hutumika kutoa baraka katika imani za kichifu akisema ndizo zilizohitimisha fursa za kugombea kwake ubunge kupitia chama hicho.
“Najisikia amani kubwa kuondoka CCM, kabla sijachukua uamuzi huu nilikuwa nikiishi kwa presha, hivi sasa nipo huru, niacheni tu kama ni ubunge sikuzaliwa nao na unaweza kuishi bila ubunge na maisha yakawa mazuri,” alisema Lembeli.
Ilivyokuwa
Juzi, Lembeli alifika katika Ofisi ya CCM Wilaya ya Kahama na kutangaza kuwa hawezi kugombea kupitia chama hicho kwa kuwa kimejaa rushwa na matukio ya wagombea kugawa kadi kwa wanachama ili wachaguliwe.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kahama, Mabala Mlolwa alielezea kusikitishwa na uamuzi huo wa Lembeli kuamua kuhama bila kushauriana na uongozi wa wilaya.
Alisema CCM inatambua mchango mkubwa aliotoa katika miaka 10 ya uongozi wake na imeshangazwa na tukio hilo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja alisema pamoja na kulisikia suala hilo, hivi sasa yupo mapumzikoni kisiasa kutokana na dhoruba kubwa ya kitaifa waliyoipata katika mchakato wa uteuzi wa mgombea urais.
“Niacheni kwanza nipumzike suala hilo nalisikia lakini muda mwingi sikuwapo. Najua suala la Lembeli kuhama litaibomoa CCM Kahama, ataondoka na wengi lakini mimi sizungumzi lolote juu ya hilo,” alisema Mgeja.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment