Mahakama ya Hakimu
Mkazi Mkoa wa Morogoro, jana ilimfutia shtaka moja kati ya matatu Katibu
wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda.
Baada ya Mahakama kufuta shtaka hilo la kwanza, sasa Ponda atatakiwa kujitetea mashtaka mawili yaliyobaki.
Mahakama hiyo iliridhika na upande wa mashtaka uliowasilisha ushahidi, hivyo Ponda atajibu shtaka la pili na tatu.
Akitoa uamuzi mdogo kama mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la, Hakimu Mary Moyo alisema Ponda ana mashtaka mawili ya kujibu.
Mashtaka
yaliyokuwa yakimkabili Ponda baada ya kufikishwa mahakamani hapo Agosti
18, mwaka 2013 ni pamoja na kutoa kauli za kuwataka Waislamu kutokubali
kuundwa kwa kamati za ulinzi na usalama za misikiti kwa vile ziko chini
ya Bakwata, ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali.
Hakimu
Moyo alisema shtaka analotakiwa kujitetea ni lile alilotenda Uwanja cha
Ndege Manispaa ya Morogoro, ambapo anadaiwa kuituhumu Serikali kupeleka
wanajeshi Mtwara kuzima vurugu za kupinga gesi kuletwa Dar es Salaam,
lakini wananchi wa huko wakaishia kuuawa, kubakwa na kuteswa kwa vile
asilimia 90 ya wakazi wake ni waislamu.
Ilidaiwa pia
kuwa Ponda aliituhumu Serikali kutopeleka polisi Loliondo baada ya
wananchi kupinga Mwarabu kupewa kipande cha ardhi ya uwindaji na hiyo ni
kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo.
Katika
shtaka la tatu, Ponda anadaiwa kuwa kauli alizotoa kuhusu wanajeshi
walioua, kubaka na kutesa wananchi na madai kuwa asilimia 90 ya wananchi
wa Mtwara ni Waislamu, zililenga kuumiza dini ya watu wengine, jambo
ambalo ni kinyume na Kifungu cha Sheria Namba 390 na Kanuni ya Adhabu
Namba 35 cha mwaka 2002.
Akifafanua, Hakimu Moyo
alisema kuwa katika kosa la kwanza, mahakama hiyo imeona Ponda hana kesi
ya kujibu kwa vile tayari shtaka hilo lilishatolewa uamuzi Mahakama Kuu
Kanda ya Dar es Salaam na kwamba mahakama ya chini haina uwezo wa
kupinga.
Baada ya hakimu huyo kutoa uamuzi huo, upande
wa utetezi ukiongozwa na Wakili Juma Nassoro uliridhika na uamuzi huo na
kwamba wako tayari kuleta mashahidi katika kesi hiyo.
Upande
wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Sunday Hyera, uliomba kupangiwa tarehe
nyingine ya kuwasilisha ushahidi wa upande wa utetezi kwa vile Wakili
Kiongozi, Bernard Kongola alishindwa kufika mahakamani kwa sababu zilizo
nje ya uwezo. Kesi hiyo itaendelea tena Agosti 7.
0 comments:
Post a Comment