Marekani yatahadharisha raia wake wanaoishi Kenya kuwa waangalifu zaidi wakati wa ziara ya rais Obama.
Serikali ya Marekani imetoa tahadhari kwa raia wake wanaoishi nchini Kenya kuwa makini na waangalifu zaidi wakati rais Obama atakapotekeleza ziara yake wiki ijayo.
Ilani hiyo ya tahadhari ilitolewa kutokana na vitisho vya mashambulizi ya kigaidi yanayoweza kutekelezwa katika maeneo mbalimbali yasiyojulikana nchini Kenya.
Idara ya ulinzi nchini Marekani pia iliwaonya raia wake na kusema kwamba wanaweza kuwa walengwa wa mashambulizi yanayoweza kutekelezwa katika shughuli za umma kama vile mkutano wa kimataifa wa ujasiriamali unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 24 hadi 26 Julai jijini Nairobi.
Hapo awali, kundi la Al-Shabaab liliwahi kuapa kuendeleza mashambulizi nchini Kenya baada ya serikali yake kushindwa kuondoa vikosi vyake vya wanajeshi walioko Somalia.
Hatua thabiti za usalama zinatarajiwa kuongezeka huku vikosi vya Kenya pamoja na maafisa wa Marekani wakishirikiana kuimarisha usalama kabla ya Obama kuwasili nchini humo.
0 comments:
Post a Comment