Hali hiyo ndani ya Bunge iliendelea kwa siku ya
pili mfululizo na mara zote kusababisha Spika kuahirisha vikao baada ya
shughuli za Bunge kushindwa kuendelea kutokana na kelele za wapinzani
wanaopinga kitendo cha uongozi kuwasilisha miswada mitatu kwa hati ya
dharura wakidai hakuna haja ya haraka hiyo.
Jana Spika Makinda, ambaye aliwahi kukumbana na
hali kama hiyo wakati wa mjadala wa sakata la Akaunti ya Escrow kwenye
Bunge la 18, aliibuka na dawa mpya na kuitumia Kamati ya Haki, Maadili
na Madaraka ya Bunge kuwaadhibu wabunge hao saba.
John Mnyika, Moses Machali, Tundu Lissu, Felix
Mkosamali na Paulin Gekul, ambao wamekuwa wakipinga hoja mbalimbali za
Serikali ikiwa ni pamoja na miswada mitatu iliyotakiwa kuwasilishwa kwa
dharura kuanzia jana, wamefungiwa kushiriki vikao kuanzia leo hadi Bunge
litakapovunjwa Julai 9.
Wabunge wengine wawili, Mchungaji Peter Msigwa na
Rajab Mbarouk wamefungiwa kushiriki vikao viwili kuanzia leo baada ya
Kamati hiyo kuwatia hatiani wawakilishi hao wote saba kwa kudharau
mamlaka ya Spika.
Wengine watatu, Joseph Selasini, Khalifa Suleiman
Khalifa na Rajabu Abdalah wanatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo leo saa
4:00 baada ya wito wa kuwataka wahudhurie jana kuchelewa.
Kikao cha jioni cha Bunge hilo, ambacho kilipokea
taarifa ya kamati hiyo ya maadili na mapendekezo ya adhabu hizo,
kilichelewa kuanza kwa saa moja na dakika ishirini kusubiri kumalizika
kwa kazi ya kuwahoji watuhumiwa.
“Mashtaka yetu yaliendeshwa kwa haraka,
hatukupatiwa muda wa kutosha kujieleza wala kumtumia wakili,” alisema
Machali baada ya Bunge kuahirishwa.
“Pamoja na kuadhibiwa, hatutaogopa kusema kuwa
miswada hiyo ina matatizo ili Watanzania wafahamu na iwapo miswada hiyo
itapitishwa malalamiko ya vizazi vijavyo juu yatakayotokea kwenye sekta
ya gesi yatakuwa juu ya Serikali na CCM.”
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alisema
ni bora kufukuzwa kuliko kuendelea kushuhudia gesi ya Watanzania ikiuzwa
kwa nguvu bila ya huruma.
“Hii ni bora kuondolewa. Hukumu haikuwa ya haki na
tungeweza kukata kukata rufaa kwenye Kamati ya Kanuni, lakini
mwenyekiti wake ni Spika hivyo basi tena, acheni wafanye wanachotaka
kukifanya,” alisema Lissu.
Mchungaji Msigwa, ambaye ni mbunge wa Iringa Mjini, alisema hata angefungiwa kushiriki vikao vyote, asingeathirika.


0 comments:
Post a Comment