Wakizungumza kwenye mkutano kati ya Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC) na viongozi wa vyama vya siasa kuhusu maadili ya
Uchaguzi jana, baadhi ya viongozi hao walitaka mkutano huo usitishwe
hadi pale CCM itakapomuonya Nape.
Wa kwanza kuibua mada kuhusu Nape, ni Mwenyekiti
wa Taifa wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi ambaye alisema hakuna
haja ya kuendelea na mkutano huo hadi NEC, Msajili wa Vyama vya Siasa na
IGP wakemee kauli hiyo.
“Hivi tutayazungumziaje maadili, mbona CCM
kimeshaonyesha kuwa hakitafuata maadili, kuna haja gani ya kuzungumzia
wakati wameshasema watafunga hata kwa goli la mkono?” alisema Dk
Makaidi.
Awali akiwa katika ziara ya Kinana wilayani ya
Sengerema, Nape alikaririwa akisema kuwa ana uhakika CCM itashinda baada
ya kuona mwitikio mkubwa wa Watanzania katika ziara hizo.
“Rangi inayoenda Ikulu ni hii (anaonyesha shati
lake la kijani ambayo hutumiwa na chama hicho). Tuna uhakika na ushindi
wa Rais. Kwa namna yoyote ile, CCM itarudi Ikulu hata kama ni kwa bao la
mkono... bao ni bao tu ili mradi refa hajaona,” alisema Nape.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva
aliwatoa wasiwasi wanasiasa hao akiwaambia kuwa Nec itafanya uchaguzi
kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu na hivyo kauli ya Nape
haiwahusu.
“Maadili tunayoyatengeneza yataanza kutumika
kuanzia Agosti 22, wakati wa kampeni, lakini iwapo kuna vurugu zinatokea
baina ya vyama sisi wala Nec hatuhusiki,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Wilbroad Slaa akichangia kipengele cha wahusika wa maadili aliitaka Nec
kuliweka Jeshi la Polisi kupitia IGP kusaini na kuwa mhusika katika
masuala ya maadili ya uchaguzi.
Hiki kipengele cha 1.3 kinawataja wahusika wa
maadili kuwa ni vyama vya siasa, wagombea, Serikali ya Jamhuri ya
Muungano na Nec pekee.
“Kutokana na uzoefu tulionao katka chaguzi
zilizopita, Jeshi la polisi ni washiriki wakubwa katika masuala ya
uchaguzi, kama jeshi hilo halitasaini maadili hayo basi kutakuwa na
matatizo makubwa katika uchaguzi huo,” alisema.
Awali akifungua mkutano huo Jaji Lubuva alivitaka
vyama vya siasa kufuata maadili, sheria na kanuni za uchaguzi, na katika
kipindi chote cha kuanza kwa kampeni hadi siku ya uchaguzi.


0 comments:
Post a Comment