Jana,Spika Anne Makinda alilazimika kuahirisha shughuli za
Bunge asubuhi baada ya wabunge wa vyama vya upinzani kupiga kelele na
hivyo kusababisha muwasilishaji wa Muswada wa Sheria ya Mafuta na Gesi
wa mwaka 2015 asisikike vizuri.
Hii ni takriban mara ya tatu kwa shughuli za Bunge
kushindikana kutokana na wabunge hao kutokubaliana na hali ya
uendeshwaji wa vikao na hoja za Serikali na hivyo kuamua kuweka
mazingira ambayo hayaruhusu kazi yoyote kufanyika.
Juzi, wabunge walidai kuwa miswada hiyo
iliwasilishwa kwenye semina na wote bila ya kujali itikadi zao za
kisiasa, waliazimia kuwa suala hilo lifanywe na Bunge lijalo. Bunge
lilipotaka kuendelea na shughuli zake ndipo kelele hizo zilipoanza na
Spika kulazimika kuahirisha kikao.
Jana tena walistukia miswada hiyo ikiwasilishwa na
walipotaka mwongozo, Spika hakusikiliza na hivyo kusababisha wabunge wa
upinzani kusimama na kuanza zogo lililosababisha kiongozi huyo wa Bunge
ashindwe kuendelea na shughuli za chombo hicho kama ilivyopangwa.
Badala yake alichukua majina ya wabunge alioona
kuwa walishiriki katika kelele hizo na kuwapeleka mbele ya Kamati ya
Uongozi kwa ajili ya kujadiliwa na kuchukuliwa hatua stahiki.
Ni kweli kwamba vurugu zinazofanywa bungeni
hazifai na kwa kweli zinakwamisha shughuli za chombo hicho muhimu.
Lakini tunadhani kuwa wabunge hao wamekosa njia nyingine ya kuhakikisha
sauti zao zinasikika.
Kwa maana hiyo, badala ya kufikiria njia za
kuwadhibiti, uongozi wa Bunge ujihoji sababu za uendeshaji wa chombo
hicho kuanza kudorora na kuweka taswira mbaya kwa jamii.
Miswada hiyo ya sheria ni muhimu kwenye jamii kwa
maana kuwa inapopitishwa inawagusa wananchi, wawakilishi wao hawana budi
kuhakikisha kuwa mchakato wa kuipitisha ni lazima uwe wa mazingira
ambayo ni muafaka kwa pande husika, yaani Serikali, wabunge na uongozi
wa Bunge.
Kwenye semina hiyo, Serikali ilitakiwa itoe
maelezo ya kina kuwashawishi wabunge kuwa kuna haja ya miswada hiyo
kupitishwa sasa badala ya baadaye.
Lakini inaonekana Serikali ilishindwa na badala
yake ikataka kutumika mbinu ya kutopokea mwongozo ili muswada usomwe na
kupita hatua hiyo ili mambo yanayofuata yafanyike kama ilivyopangwa.
Huu si utaratibu mzuri na hautakiwi kutumika
kwenye dunia ya sasa inayoendelea kujaa watu walioerevuka na wenye
kuhoji kila kitu. Kinachotakiwa mbele ya jamii kama hiyo, ni majibu na
maelezo ya kutosha kushawishi watu umuhimu wa jambo lililo mbele yao.
Wabunge kutoka upinzani wanajua kuwa kwa idadi ni
wachache hivyo Serikali inapowasilisha jambo ni rahisi kwa wenzao
wanaotoka chama kinachotawala, kulikubali hata kama halifai au lina
kasoro. Ndiyo maana wameamua kutumia mbinu hiyo ya kelele.


0 comments:
Post a Comment