Ingawa ibara yote ya 75 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania inaelekeza jinsi majimbo ya uchaguzi yatakavyogawanywa, kifungu
kidogo cha (4) ndicho hasa kimezingatiwa kwa kuwa kinasema wazi kuwa
Nec inaweza kutekeleza jukumu hilo mara kwa mara angalao kila baada ya
miaka kumi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Nec katikati ya mwezi huu
majimbo hayo yako katika makundi mawili; mosi, yaliyoanzishwa kwa kigezo
cha ongezeko la halmashauri na pili, yaliyoanzishwa kwa kigezo cha
ongezeko la idadi ya watu.
Nec ilitaja majimbo ambayo yalianzishwa kwa kigezo cha halmashauri
kuwa ni 20 na kuyaorodhesha kuwa ni Handeni Mjini, Nanyamba, Makambako,
Butiama, Tarime Mjini, Tunduma, Nsimbo, Kavuu, Geita Mjini, Mafinga
Mjini, Kahama Mjini, Ushetu, Nzega Mjini, Kondoa Mjini, Newala Mjini,
Mbulu Mjini, Bunda Mjini, Ndanda, Madaba na Mbinga Mjini.
Majimbo yaliyoanzishwa kwa kigezo cha idadi ya watu ni sita na
yalitajwa kuwa ni. Mbagala (Dar es Salaam), Kibamba (Dar es Salaam),
Vwawa (Mbeya), Manonga (Tabora), Mlimba (Morogoro) na Ulyankulu
(Tabora).
Wakati majimbo haya mapya yanatangazwa maeneo mengi nchini yalikuwa
yemekwisha kukamilisha kazi ya kuandikisha wapiga kura katika Daftari
la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa kielektroniki wa kutambua alama za
mwili (Biometric Voters Registration –BVR). Kazi hiyo ingali inaendelea
katika mkoa wa Dar eas Salaam.
Wakati kazi hii ikiendelea, wananchi wengi wanakabiliwa na
changamoto kubwa, kwamba hawajui baada ya kutangazwa majimbo haya mapya
wao wanaangukia wapi. Kuna jimbo moja ambalo limegawanywa kuwa mawili,
na pengine hata katika kuanzisha halmashauri hizo ipo mipaka mipya
imetengwa ili kuhalalisha maeneo ya kiutawala kwa kuanzishwa kwa mamlaka
hizo. Mambo haya yote yanafanyika wakati wananchi ambao ni walengwa
wengi wakiwa hawajui wanaangukia wapi.
Mathalan, kwa mkoa wa Dar es Salaam majimbo mawili yamegawanywa,
haya ni Ubungo na kutoa Ubungo na Kibamba, wakati Temeke na Kigamboni
kwa pamoja yamezaa jimbo la Mbagala. Katika mabadiliko hayo, kuna
mkanganyiko mkubwa wa mipaka. Wapo wananchi wengi ambao hawajui kwa sasa
wanaangukia wapi.
Tunafikiri ni vema na haki kama Nec itachukua jukumu ya kufafanua
kwa kina kwa wananchi kwa njia ya mabango, vipeperushi na matangazo
kwenye vyombo vya habari ili kila mwananchi ajijue yuko wapi.
Jambo hili ni muhimu sana hasa inapotiliwa maanani kwamba maeneo
mengi ya makazi katika miji yetu hayajapimwa, watu wamejijengea tu
holela, kwa maana hiyo ni rahisi watu kujikuta wakivutwa huku na huko
kwa maslahi ya kisiasa kama mipaka hii haitakuwa bayana kwa wananchi.
Kwa kuwa kugawa majimbo ni jukumu la kikatiba la Nec, tunaamini
kwamba hata kuwaelekeza na kuwaelemisha wananchi juu ya mipaka ya
majimbo husika pia litakuwa ni jukumu mojawapo kubwa la Tume ili
wananchi wajue fika watawapigia kura kina nani kwa maana ya wabunge na
madiwani wakati wa uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
Tunajua kwa sasa Nec inakabiliwa na mambo mengi katika kufanikisha
mchakato wa uchaguzi mkuu mwaka huu. Pamoja na majukumu hayo, tunaamini
elimu kwa raia juu ya mipaka mipya ya majimbo ni jambo la umuhimu pia.
Ni kwa kutambua ukweli huo, tunaihamasisha Nec ijipange kuhakikisha
kwamba mipaka ya majimbo mapya ya uchaguzi inajulikana vilivyo kwa
wananchi wote.
0 comments:
Post a Comment