Kama ilivyo ada, kipindi hiki huwa kinaelezewa kuwa ni cha mavuno
kwa baadhi ya watu. Kwamba. wapo wafuasi wa vyama vya siasa hukitumia
kujiingizia fedha kwa njia haramu ya rushwa, wakinufaika kutoka kwa
baadhi ya watia nia wenye uchu wa madaraka unaochochewa na nguvu ya
fedha.
Wafuasi wa vyama wasiozingatia maadili wamejiweka tayari kwa
mavuno, na wengine wameshaanza kuvuna fedha haramu za rushwa kwa
minajili ya kufanikisha miradi ya watu wanaoamua kufanya kila wawezalo
kuhakikisha kuwa wanateuliwa kuwa wagombea kwa ajili ya uchaguzi mkuu
ujao.
Hakika, watu wa aina hii hawastahili kuachwa waendelee na vitendo
hivi haramu. Hatua madhubuti zinatakiwa kuchukuliwa mara moja katika
kuwadhibiti ili mwishowe taifa lisijikute likiwa na viongozi wenye
kukumbatia rushwa.
Kwa mfano, inaelezwa kuwa katika maeneo yenye ushindani mkali kwa
nafasi za ubunge wa viti maalum kama jijini Dar es Salaam, baadhi ya
watia nia wanaotaka kuteuliwa kwa nafasi hizo wamekuwa wakimwaga kiasi
kikubwa cha fedha.
Wengine wanadaiwa kuwa tayari hivi sasa wamekuwa wakiwanunua
wanachama wenzao wenye kushiriki uteuzi kwa kuwapatia dau la kuanzia Sh.
200,000 kwa kila mmoja na kuendelea. Lengo la wahongaji ni kupita
kirahisi katika hatua ya mchujo.
Kadhalika, wapo watia nia wa kugombea katika majimbo wamekuwa
wakitumia fedha nyingi pia kwa kuzigawa kwa wapiga kura ndani ya vyama
vyao. Tatizo hili linadaiwa kuvikumba vyama vingi vya siasa katika
kipindi hiki, ingawa tuhuma kuhusu jambo hili zinatajwa kuwa katika
kiwango cha juu zaidi ndani ya chama tawala, CCM.
Kwa hatua ya sasa, siyo nia yetu kutaka kujua ni nani hasa amekuwa
akitoa rushwa na ametenda dhambi hiyo kwa kushirikiana na nani. Hata
hivyo, tunadhani kwamba ni vizuri kwa kila mpenda demokrasia na aliye
mfuasi wa maadili akalaani vitendo vya aina hii kwa nguvu zote.
Tungependa kuona kuwa jamii inashirikiana kwa kila hali kuhakikisha
kuwa hakuna makada wa vyama wanaopitishwa kuwa wagombea kwa kutumia
'mbeleko' ya rushwa kwani kuruhusu jambo hilo ni sawa na kuliweka taifa
njiapanda. Bali, uwezo wa kujieleza wa kila mtia nia na uwezo wa
kutambua changamoto za eneo husika na kuainisha mipango ya
kuzishughulikia kero zinazowakabili ndiyo sifa mojawapo muhimu
zinazopaswa kuwa kigezo cha uteuzi rasmi wa wagombea.
Tunasisitiza hili kwa vile tunajua kuwa dhamira ya mgombea yeyote
mwenye nia njema huwa ni kuwaongoza wananchi wenzake katika safari ya
maendeleo, wakitoka hatua moja hadi nyingine. Kinyume chake, wagombea
wasiokuwa na dhamira ya kuendeleza maeneo wanayotaka kugombea na badala
yake kutanguliza mlungula wa namna yoyote ile huwa hawafai.
Kwa kutambua yote hayo, ndipo sisi tunapoona kwamba sasa kuna kila
sababu kwa wafuasi wa kila chama kuipa kisogo rushwa. Badala ya
kuwakumbatia watembeza fedha, wawaepuke na kuwaadhibu kwa kuwanyima kura
za uteuzi.
Ni imani yetu vilevile kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) haijalala. Ingali macho, ikijua kungali mapema kuwapo
kwa vitendo vya rushwa katika mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya
vyama, hasa katika kipindi hiki cha kukaribia uchaguzi. Kwa sababu hiyo,
tunaamini kuwa taasisi hii (Takukuru) itakunjua makucha kwa kusambaza
maafisa wake kwa wingi kadri iwezekanavyo ili kuhakikisha kuwa watoaji
na wapokeaji wa rushwa wanakamatwa na kufikishwa mbele ya mkono wa
sheria.
Shime, rushwa isipewe nafasi. Wafuasi wa vyama washirikiane na
Takukuru kwa kutoa taarifa muhimu zitakazosaidia kukamatwa kwa wote
wanaotumia fedha kama nyenzo ya kupata nafasi ya kuteuliwa na vyama vyao
ili wagombee katika uchaguzi mkuu Oktoba 25, 2015.
0 comments:
Post a Comment