Jitihada za Serikali katika kupambana na uhalifu
wa mitandao imeungwa mkono kutokana na baadhi ya vyuo kuanzisha mitalaa
yenye somo la ulinzi wa mitandao.
Moja ya jitihada za
serikali katika kukabiliana na changamoto hiyo ni kupeleka muswada wa
sheria ya uhalifu wa mtandao ya mwaka 2015 katika mkutano wa 19 wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ulipitishwa na Bunge
hilo.
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknologia,
Profesa Makame Mbarawa anasema, kukua kwa kasi kwa matumizi ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kumeleta mafanikio kwa
kuongezeka kwa biashara zinazotumia huduma za mawasiliano, fedha na
matumizi ya mitandao.
Anaeleza kuwa hayo ni mapinduzi
ya maendeleo kwa kutumia teknolojia lakini kwa upande mwingine yameleta
changamoto nyingi katika jamii ikiwamo kuibuka kwa uhalifu na kuibua
makosa mapya ya jinai.
Makosa hayo, anasema
yanajumuisha uhalifu wa mitandao ambapo simu za mkononi, kompyuta au
mifumo ya kompyuta hutumika kama nyenzo za kutenda uhalifu huo.
Mifano
ya makosa hayo ni pamoja na wizi wa fedha kwa njia ya mtandao,
ugaidi, maudhui potofu yanayosababisha mmomonyoko wa maadili,
uharibifu wa miundombinu muhimu ya Taifa ikiwamo mkongo wa Taifa wa
Mawasiliano.
Mtaalamu wa Ulinzi wa Mitandao, Ezekiel
Mpanzo anasema tatizo la wizi wa mitandao limekuwa kubwa na kusababisha
hasara kwa benki pamoja na wananchi.
Mpanzo ambaye pia
ni Mkuu wa Chuo cha Teknolojia na Uongozi cha Kilimanjaro, anasema kwa
upande wa vyuo vilivyopo chini ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi
(Nacte) pamoja na vyuo vikuu wamegundua tatizo hilo na wamejaribu
kutengeneza mtalaa ambao una somo la kuzuia wizi huo.
“Tumetengeneza
mtalaa mzuri na kuingiza somo la ulinzi wa mtandao. Tumeuandaa sisi
wenyewe na kuupeleka Nacte na wameupitisha, kwa hiyo tunaamini kwamba
utasaidia Taifa kupunguza tatizo hilo,” anasema Mpanzo.
Anasema
njia nyingine ya kuzuia tatizo hilo ni wataalamu wa hapa nchini
kujiunga na vyama vya kuzuia uhalifu wa mitandao duniani. “Wataalamu wa
hapa nchini, wakijiunga na vyama hivyo, vikiwamo Ethical Hacking na
Sisco, itasaidia kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu wanazotumia wahalifu
duniani kote kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknologia,”
anabainisha Mpanzo.
Lengo lao, anasema ni nchi kuwa na
wataalamu wengi watakaosaidiana na Serikali pamoja na taasisi
mbalimbali, kukabili tatizo la wizi kwa kutumia mitandao.
Anasemakatika
mwaka 2010 na robo ya mwaka 2013 Tanzania ilipoteza Sh9.8 bilioni
kutokana na wizi huo ambao ulifanywa katika mashine za kutolea fedha
maarufu kama ATM.
Hivi karibuni, Jijini Arusha
ulifanyika mkutano wa kujadili mbinu za kuzuia wizi kwa kutumia mitandao
katika nchi za Afrika Mashariki ambapo ilitolewa ripoti kuhusiana na
vitendo hivyo.
Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima anabainisha kuwa hapa nchini kuna
kesi zaidi ya 300 za uhalifu wa mitandao ambazo zinachunguzwa na baadhi
ziko kwenye hatua ya kufikishwa mahakamani.
Katika
mkutano huo pia ikabainika kuwa wizi huo umekuwa ukifanyika kirahisi
kutokana na nchi za Afrika Mashariki kutokuwa na wataalamu wa kutosha
katika kukabili vitendo hivyo haramu.
Wadau wengi wa mitandao kwenye mkutano huo wanaweka wazi kuwa kuna umuhimu wa kubadilishana uzoefu kwa wataalam.
Hii
inatokana na ripoti iliyotolewa na Kampuni ya Kaspersky lab ambayo
ilibainisha kuwa genge la wahalifu wa mtandao lilifanikiwa kuiba
mamilioni ya Dola za Marekani kutoka kwenye akaunti za wateja wa benki
1,000 katika mataifa 30 kati ya mwaka 2014 na 2015.
Wizi huo unaonekana ulianza mwaka 2013 na bado unaendelea kwenye benki mbalimbali, huku kukiwa na mbinu finyu katika kuukabili.
Ripoti
hiyo ilitoa mfano wa mbinu za genge la Carbanak, linatumia mbinu ya
kuambukiza virusi kwenye mashine na kompyuta za benki ikiwamo kamera za
CCTV ili kunakili kila kitu kinachoandikwa kwenye komputa.
Ripoti
hiyo inaelezea mbinu mpya za wahalifu mtandao wanazotumia kudukua
nambari za akaunti za wateja za siri kabla ya kuingia na kuiba fedha.
Kwa
mujibu wa ripoti hiyo, benki katika mataifa 30 yakiwamo, Russia,
Marekani, Ujerumani, China, Ukraine na Kanada yameathirika kwa asilimia
kubwa.
Kaspersky imesema kuwa wizi huo ulianza mwaka wa
2013 na bado unaendelea hata leo kwani hivyo benki nyingi zinapaswa
kuwa makini kwa sababu bado uhalifu huo unaendelea.
Taarifa
inaeleza kwamba genge la wahalifu mtandao limefanikiwa kuiba mamilioni
ya Dola za Marekani kutoka kwenye akaunti za wateja wa benki 100 katika
mataifa 30 kati ya mwaka 2014 na 2015.
Genge hilo la
wezi, lililoanzia shughuli zake nchini Urusi, Ukraine na Uchina. Kwa
mujibu wa ripoti hiyo benki katika mataifa 30, zikiwamo za Russia,
Marekani, Ujerumani, China, Ukraine na Canada.
Uchunguzi
mbalimbali wa kimataifa unaonyesha kuwa wezi wamekuwa werevu kiasi
kwamba, huweza kutumia teknolojia kupata taarifa za siri za watumiaji wa
kompyuta zilizounganishwa kwenye mitandao.
Wanatumia
programu mbalimbali zinazoitwa virusi vya kompyuta kupata taarifa hizo.
Virusi hao ni kama vile trojans, worms, viruses, hacktools, rootkits na
hadware.
“Siku hizi kuna uhusiano wa kampuni hasa kati
ya maharamia wa njia za mitandao na kampuni au vikundi vinavyojihusisha
na jinai. Hawa ndio wanaojihusisha na jinai na ndio mara nyingi wanakuwa
ni chanzo cha kuwezesha kusambaza mafanikio ya wizi kwa njia ya
mtandao,” anasema Daniel Kamau kutoka kampuni ya inayojihusisha na
utengenezaji wa kompyuta pamoja na programu zake ya Microsoft.
Baadhi
ya mitandao inayoibuka na kulaghai kwa kuwataka wananchi, kutoa taarifa
zao muhimu za kibenki, jambo ambalo linahatarisha usalama wa fedha zao
zinazohifadhiwa na benki hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa
CRDB, Dk Charles Kimei anasema kuwa kumeibuka mchezo kwa baadhi ya
mitandao ya kijamii, ikijaribu kuwalaghai wateja kwa kuwaomba taarifa za
akaunti zao ili kufanya uhalifu.
Alisisitiza wananchi
wanatakiwa kuwa makini na kundi hilo, wasikubali kudanganyika kwa kutoa
taarifa zinazohusiana na nyaraka nyeti za benki zao na kusisitiza kuwa
ni marufuku kutoa taarifa hizo hata kwa wafanyakazi wa benki.
Kauli
ya Kimei inawiana na tamko la mitandao ya simu linalowahadharisha
wateja wao kutotoa taarifa zao, hasa namba ya siri za akaunti zao za
fedha, hata kama wanaozitaka watajitambulisha ni wafanyakazi wa mitandao
husika.
Hali hii inaashiria kuwa wahalifu wanatumia
teknolojia ili kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu. Hii inaashiria
wazi kwamba Tanzania nayo inapaswa kuweka mkakati wa hali ya juu wa kuwa
na wataalamu wa kutosha ili kukabiliana na tatizo hilo.
0 comments:
Post a Comment