Ukawa, inayoundwa na vyama vya Chadema, CUF,
NCCR-Mageuzi na NLD, imekubaliana kusimamisha mgombea mmoja kuanzia
ngazi ya urais hadi diwani na viongozi wa vyama hivyo wameshakutana mara
kadhaa kuzungumzia kugawana majimbo kulingana na nguvu ya chama kwenye
eneo husika.
Hata hivyo, vimeshindwa kumalizia kazi hiyo
kutokana na kutokamilika kwa mgawanyo wa majimbo kama NEC ilivyoahidi
Mei 12 kuwa majimbo mapya kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25
yangetangazwa Juni 30.
Akizungumza jana, Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Chadema aliitupia lawama NEC akisema wakati huu ilitakiwa kuwa
imeshamaliza suala la majimbo na kushughulikia mambo mengine.
“Tunataka kutengeneza ratiba ya mpango kazi,
lakini tunashindwa. Tunataka tujue majimbo mapya ili twende huko, lakini
sasa tunashindwa na muda unakwenda,” alisema Mbowe.
Akizungumzia ukimya wa kutangaza majimbo hayo
licha ya kusema ingefanya hivyo Juni mwishoni, Mwenyekiti wa NEC, Jaji
Damian Lubuva alisema hadi sasa Tume hiyo haijakamilisha ugawaji wa
majimbo lakini bado wanaendelea na mchakato huo.
Alisema Tume yake imeamua kugawa majimbo hayo kwa
kuzingatia vigezo mbalimbali, ikiwamo idadi ya watu, upatikanaji wa
mawasiliano, hali ya kijiografia na kanuni za uchaguzi wa Rais na
wabunge za mwaka 2010.
Jaji Lubuva pia alisema Tume itayagawa majimbo
hayo kwa kuzingatia uwepo wa miundombinu bora, hali ya kiuchumi kwa
kuweka uwiano kati ya eneo moja na jingine, mawasiliano ya simu na
vyombo vya habari kwa ajili ya kupata mwakilishi atakayeharakisha
maendeleo katika eneo husika.
Wakati ikisuasua kutangaza majimbo mapya ya
uchaguzi, NEC pia inakabiliwa na kibarua kingine cha kumalizia
uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Kazi hiyo imekumbwa na matatizo kadhaa na
inatakiwa ikamilishwe katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, lakini
imeahirishwa kutokana na kuchelewa kwa mashine zinazotumika za
teknolojia ya mfumo wa kuchukua alama na taswira za mpigakura (Biometric
Voters Registration).
Jaji Lubuva alisema kuwa kuna baadhi ya majimbo ambayo ni makubwa, jambo ambalo alisema linatokana na ongezeko la watu nchini.
Ugawaji wa majimbo unatakiwa kufanyika mara kwa mara au angalau mara moja baada ya miaka 10.


0 comments:
Post a Comment