Tangazo lililotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji
(Ewura), bei ya petroli imeongezeka kwa Sh. 232 ambayo ni sawa na
asilimia 11.82, dizeli Sh. 261 (asilimia 14.65) na mafuta ya taa Sh.
369, sawa na ongezeko la asilimia 22.75.
Ewura ilieleza sababu za kuwapo kwa mabadiliko hayo kuwa ni
kuendelea kudorora kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani na
pia kuanza kutumika kwa tozo mpya za mafuta hayo zilizopitishwa bungeni
kupitia bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Ni wazi kwamba mabadiliko haya ni pigo kubwa kwa wananchi walio
wengi. Ni kwa sababu mafuta hugusa karibu kila nyanja. Ndiyo mhimili wa
sekta ya usafiri wa watu na bidhaa. Mafuta hutumika pia kulainisha
mitambo viwandani na pia kuendesha mitambo ya kufua nishati ya umeme.
Kwa kutambua yote hayo, ndipo sisi tunapoona kwamba sasa kuna
umuhimu mkubwa kwa serikali kuangalia ni kwa namna gani kuporomoka kwa
shilingi kila uchao kutadhibitiwa kivitendo ili kuepusha bei ya mafuta
kupanda na mwishowe kuathiri pia bidhaa nyingine.
Sisi tunaamini kwamba kwa kuchukua hatua za dhati za kulinda
thamani ya shilingi, ndipo makali ya maisha yatokanayo na kupanda kwa
bei ya mafuta na bidhaa nyingine yatadhibitiwa.
Sisi tunaamini kuwa jambo muhimu zaidi la kulifanyia kazi kwa sasa ni kulinda thamani ya shilingi yetu.
Tunasisitiza hili kutokana na ukweli kuwa athari za kuporomoka kwa
shilingi ziko wazi, hasa katika kuchangia ongezeko la bei ya mafuta. Kwa
mfano, takwimu zinaonyesha kuwa bei ya mafuta ghafi ya petroli katika
soko la dunia imekuwa ikiporomoka katika miezi ya hivi karibuni. Mei
Mosi mwaka huu, pipa moja la petroli ghafi lilikuwa likiuzwa kwa dola za
Marekani 64.13. Bei hiyo ilishuka hadi kuwa dola za Marekani 60.54
kufikia Juni 22 mwaka huu. Hata hivyo, nafuu hiyo haionekani sasa nchini
kutokana na kuporomoka kwa thamani ya shilingi yetu.
Udhaifu wa shilingi unadhihirishwa na ukweli kuwa wastani wa
thamani ya shilingi Mei mwaka huu dhidi ya dola ulikuwa Sh. 1,955.72,
lakini mwezi uliofuata wa Juni, iliporomoka kiasi cha kubadilishwa kwa
zaidi ya Sh. 2,300 huku wastani wa jumla kwa mwezi huo (Juni) ukiwa Sh.
2,096.
Kwa sababu hiyo, ni vizuri serikali kupitia mamlaka zake ikahakikisha kuwa thamani ya shilingi inalindwa vya kutosha.
Vyanzo vya kuporomoka kwa shilingi vinafahamika. Mathalan,
kuendelea kuagiza bidhaa nje ya nchi huku tukijua kuwa zinaweza
kuzalishwa nchini ni kuiangusha shilingi. Kama ilivyowahi kuelezwa mara
kadhaa bungeni na nje ya bunge, hakuna sababu ya kuagiza vyakula kama
mchele na ngano wakati tuna ardhi kubwa na yenye rutuba ya kutosha
kuzalisha mazao hayo nchini. Hakuna sababu pia ya kuagiza kutoka nje
bidhaa kama vibiriti, mabati, misumari, saruji, vijiti vya kuchokonolea
meno na vitambaa vya kufutia jasho kwani vyote hivyo vinaweza kuzalishwa
nchini.
Isitoshe, matumizi holela ya dola yanapaswa pia kudhibitiwa kwani
kutofanya hivyo ni sawa na kuongeza mahitaji ya fedha hizo za kigeni na
hivyo kupunguza thamani ya shilingi yetu. Kwa mfano, kuna haja gani ya
kuruhusu taasisi kama za elimu kutoza ada kwa dola? Kwa nini kuna hoteli
zinaachwa ziendeshe shughuli zao nchini kwa kutumia sarafu ya dola huku
tukijua wazi kwamba kufanya hivyo ni kuporomosha shilingi na mwishowe
kuathiri uchumi wetu? Kwa nini wamiliki wa baadhi ya nyumba wanaachwa
watoze kodi kwa kutumia fedha za kigeni?
Hakika, yapo maeneo mengi ambayo tunaweza kuyafanyia kazi na
kuimarisha shilingi yetu. Sheria za kukabiliana na watu wanaoopuuza
shilingi na kulazimisha matumizi ya dola katika biashara ya bidhaa na
huduma zipo. Mamlaka za usimamizi ziingilie kati na kuwachukulia hatua
wale wote wanaokiuka sheria zinazolinda shilingi yetu.
Ikumbukwe kuwa kutofanya jitihada za kulinda shilingi yetu ni sawa
na kukaribisha mfumuko mkubwa wa bei ya mafuta ya petroli na mwishowe
huduma na bidhaa nyingine zote. Kila mmoja aamke sasa na kutekeleza
wajibu wake sasa kwani vinginevyo, kama shilingi itaendelea kwua dhaifu,
ni wazi kuwa bei za bidhaa muhimu kama mafuta ya petroli zitaendelea
kupanda kila uchao.


0 comments:
Post a Comment