WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali katika sekta ya afya, wanatarajia kuendesha kampeni ya
uhamasishaji wa uzazi wa mpango kwa jamii katika maeneo ya mabaa na
vilabu vya pombe mkoani Kigoma.
Meneja Mawasiliano wa Shirika la World Lung Foundation, Victoria
Marijani alisema hayo katika mahojiano na waandishi wa habari wakati wa
kikao cha wadau kujadili njia mbalimbali za kuwa na mpango wa pamoja na
kuendesha kampeni za uzazi wa mpango mkoani Kigoma.
Alisema mkakati huo, unalenga kufikia malengo ya kitaifa ya asilimia
60 ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango ili kuongeza uelewa kwa
wananchi ambao wakati mwingine hawafikiwi katika kampeni zinazofanyika.
Hata hivyo, Meneja huyo wa World Lung Foundation, alisema umekuwa na
mafanikio kiasi katika matumizi ya njia za uzazi wa mpango tangu kuanza
kwa kampeni zinazoendeshwa na shirika hilo na watu wameanza kujitokeza
katika kutumia njia hizo za uzazi wa mpango.
Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma, Dk Leonard Subi alisema bado kuna uelewa
wa chini kwa wananchi wa mkoa huo katika kujua elimu ya afya ya uzazi na
matumizi ya njia za uzazi wa mpango, ambapo kwa sasa asilimia 14 ya
wananchi wa mkoa huo ndiyo wanaotumia njia hizo.
Sambamba na hilo, Dk Subi alisema dini, mila na desturi pia ni
kikwazo kwa wananchi katika kutumia njia za uzazi, ambapo wananchi wengi
wanaamini kwamba kila mtoto anakuja na riziki yake aliyoandikiwa na
Mungu.
Alisema kufanyika kwa mkutano huo wa pamoja wa wadau wanaotoa huduma
za afya katika sekta hiyo, kutasaidia kuzifanya kampeni hizo kuwa na
mafanikio na kuongezeka kwa uelewa kwa wananchi katika kutumia njia za
uzazi wa mpango.
Dk Wilfred Mongo kutoka shirika la EngenderHealth, alisema kuwa bado
hakuna wataalamu wa kutosha wa kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi ya
njia za uzazi wa mpango na kwamba kilichopo sasa ni watu wengi kutoa
habari kuhusu jambo hilo kuliko kutoa elimu.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment