Image
Image

Kibamba ahofia TAKUKURU.

MTAFITI na mchambuzi wa masuala ya demokrasia kanda ya Afrika Mashariki, Deus Kibamba ametilia shaka umakini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufuatia ukamataji makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati huu chama hicho kikiendesha kura za maoni za kutafuta wagombea ubunge na udiwani kwa uchaguzi mkuu ujao. Anaandika Pendo Omary … (endelea).
Kampeni za waombaji ridhaa pamoja na kura za maoni za makada wa CCM zimeshuhudiwa kugubikwa na matumizi makubwa ya fedha, kiasi cha TAKUKURU kuwatia mbaroni viongozi na wagombea wakiwa na mifuko ya mamilioni ya shilingi zilizohisiwa kama za kugawa rushwa kwa wapiga kura.
Akizungumza na MwanaHALISI Online leo, Kibamba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), amesema “Takukuru ni kibogoyo. Haina nguvu na haiwezi kupambana na rushwa hasa katika kipindi hiki. Ninatilia shaka sana umakini wake kama chombo cha kudhibiti rushwa nchini.”
Kibamba amesema wakati watumishi wa taasisi hiyo wakijitahidi kushika watuhumiwa wa rushwa miongoni mwa makada wa CCM, kesi hazionekani, kwa kuwa zinaishia mikononi mwa viongozi wakuu wa taasisi.
“Vijana wake wanawakamata watuhumiwa na kuwahoji. Wakati wakiandaa mashtaka, wanapokea vimemo vya viongozi wa juu wa CCM wakitaka kusitisha mashtaka, ndiyo ninaposema nina shaka na umakini wa taasisi hii,” amesema.
Kibamba amesema matokeo ya kukithiri kwa rushwa katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM, ni watu wenye sifa ya uongozi kukosa nafasi hiyo, huku wale wagawa rushwa wengine wakiwa ovyo tu, wanapenya kwa nguvu ya fedha zao. “Hawa ndio wanakuja kuwa viongozi wa wananchi, ni jambo la hatari kwa taifa.”
“Ili Takukuru ifanye kazi kwa ufanisi lazima ikatae kwa namna yoyote ile uingiliwa kazi zake,” amesema.
Vyombo vya habari vimeripoti matukio ya kukamatwa viongozi kadhaa wa CCM wakituhumiwa kuhusika na rushwa. Rushwa imelalamikiwa na baadhi ya wagombea wenyewe huku baadhi yao wakijitetea kuwa wamepakaziwa tu.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM taifa, Nape Nnauye alihojiwa kwa saa tano mjini Mtwara baada ya Takukuru Mkoa kutuhumu kuwa alikuwa anakusudia kugawa rushwa kwa wapigakura wa jimbo la Mtama alikoomba kugombea.
Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa CCM na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Kata ya Goba, Pili Mustafa wamehojiwa kwa tuhuma kama hizo. Wakati Nape alikutwa na zaidi ya Sh. 3 milioni, Pili alikutwa na Sh. 1.3 milioni.
Rehema Luwanja anayegombea udiwani Kata ya Goba alikamatwa na Sh. 95,000 akituhumiwa kugawa tayari Sh. 110, 000. Katibu wa Itikadi Kata ya Kibamba, Babu Kimanyo alikamatwa akiwa na Sh. 252,000 akiwa ameshagawa Sh. 330,000.
Katibu Kata ya Kibamba, Elias Nawera anaegombea ubunge jimbo la Kawe na Siraju Mwasha anayegombea udiwani kata ya Msigani nao walikamatwa.
Viongozi wengine ni Mweka Hazina wa Chama cha Walimu Taifa (CWT), Mohamedi Utali anayegombea ubunge jimbo la Lindi Mjini, na mbunge wa Viti Maalumu Fatuma Mikidadi wa Mchinga.
Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kinondoni, Denis Manumbu amenukuliwa akisema pamoja na waliokamatwa katika wilaya yake, alipokea malalamiko 28 ya mienendo ya tushwa kuhusiana na kura za maoni za CCM.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment