JIJI la Dar es Salaam limevuka lengo la uandikishaji wapiga kura
katika daftari la kudumu la wapiga kura, licha ya zoezi hilo kuanza kwa
kusuasua.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika hili, inastahili pongezi
kubwa. Tunasema hivyo kwa kuwa, kwa mara ya kwanza kutumika kwa mfumo
mpya wa kielektroniki ujulikanao kama Biometric Voter Registration (BVR)
imeweza kufanikiwa kuvuka lengo karibu kila mkoa ilipoandikisha
Watanzania kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Kwa Dar es Saalam pekee, lengo lilikuwa kuandikisha watu 2,810,423,
lakini hadi kukamilika kwake, watu 2,845,256 ambao ni sawa na asilimia
101.2 walikuwa wameandikishwa.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu, Damian Lubuva alisema juzi katika
taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari kuhusiana na kukamilika
kwake mkoa wa Dar es Salaam kwamba hadi Agosti 4 mwaka huu, wananchi
waliojiandikisha katika wilaya ya Kinondoni walikuwa 1,157,6617 sawa na
asilimia 105, ambapo lengo lilikuwa 1,102,565.
Alisema wilaya ya Temeke iliandikisha wapigakura 886,564 sawa na
asilimia 98.9 wakati lengo lilikuwa watu 896,142. Akasema wilaya ya
Ilala imeandikisha wapigakura 886,564 sawa na asilimia 98.9 na lengo
lilikuwa ni 811,716.
Tume imetangaza kukamilika rasmi kwa zoezi hilo kwa mkoa wa Dar es
Salaam na hivyo kuhitimisha rasmi uandikishaji wa wapiga kura kwa
kutumia mfumo wa kielektroniki wa BVR kwa nchi nzima bila kuwepo na
malalamiko ya watu waliokuwa wana nia ya kujindikisha kushindwa kufanya
hivyo kwa sababu zozote zile.
Wapo waliokuwa wakibeza zoezi zima, kabla halijaanza, lilipoanza
mikoani hadi lilipohitimishwa Dar es Salaam, lakini Tume imefanikiwa
kulipita lengo la uandikishaji. Haya ni mafanikio makubwa katika nchi
changa kama hii ambayo teknolojia haijakua vya kutosha.
Tume imeweka wazi kwamba sasa kazi iliyopo ni kuliweka wazi daftari
hilo la awali ambapo hadi sasa tayari mikoa 19 imekwishapelekewa.
Akasema mikoa mingine ikiwemo Zanzibar na Dar es Salaam mchakato wa
kuandaa daftari la awali unaendelea na unatarajiwa kukamilika muda si
mrefu kuanzia sasa baada ya uandikishaji kukamilika.
Ni ya kufanya hivyo ni kutoa fursa kwa wale waliojiandikisha kuweza
kusahihisha taarifa zao, kuhamisha taarifa za wapia kura waliohama
kutoka kata au jimbo moja kwenda kata au jimbo lingine, kutoa kadi kwa
wapiga kura waliopoteza kadi zao na kuangalia iwapo taarifa za mpiga
kura aliyejiandikisha zipo kwenye daftari.
Sifa nyingine ambayo Tume imeainisha ni kuweka pingamizi kwa jina au
taarifa za mpiga kura asiye na sifa ya kuwemo katika daftari la kudumu
la wapiga kura.
Ni ukweli ulio wazi kwamba uandikishwaji katika mkoa wa Dar es Salaam
na nchi nzima umefanyika na kukamilika kwa mafanikio makubwa mbali na
changamoto za hapa na pale zilizojitokeza hasa katika hatua za mwanzo za
uandikishaji.
Tunaipongeza Tume hiyo kwa mafanikio haya na tunaamini Uchaguzi Mkuu
ujao utafanikiwa vile vile kwa asilimia kubwa kwa maana ya kwamba watu
wengi watajitokeza kupiga kura.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment