SEMA wewe. Ndivyo unavyoweza kutamka baada ya maelfu ya wakazi wa
Jiji la Mwanza kujitokeza kumpokea mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa jana.
Vilevile, Jeshi la polisi mkoani hapa lililazimika kupiga mabomu ya
machozi kuwatawanya wafuasi wa Chadema na vyama vingine vinayounda
UKAWA ambao walikuwa wamefurika uwanja wa ndege wa Mwanza.
Mabomu hayo yalianza kupigwa ya saa 6:20 mchana. Mabomu hayo
yalipigwa baada ya wafuasi hao kutaka kuingia kwa nguvu ndani ya uwanja
wa ndege kumpokea Lowassa.
Kutokana na hali hiyo, wafuasi hao walilazimika kusimama nje ya lango la kuingia uwanjani.
Polisi walilazimika kuchukua uamuzi huo, baada ya wafuasi hao ambao
walikuwa na magari na pikipiki kutaka kuingia uwanja baada ya kuwazidi
nguvu walinzi wa uwanja huo.
Msafara wa Lowassa:
Lowassa aliwasili uwanjani hapo saa 7:30 mchana na kupokewa na viongozi mbalimbali wa Ukawa.
Baada ya kusalimiana na viongozi hao msafara wa Lowassa uliondoka uwanja wa ndege wa Mwanza ukiongozwa na pikipiki.
Moja ya kituko kikubwa kilichotokea ni wakati wafuasi hao walipoamua
kusafisha barabara kwa maji na kuimba wa salamu unaotumiwa na Chadema wa
‘Peoples Power’.
Hatua hiyo iliwafanya polisi kutaka kuzuia maandamano hayo lakini
kila baada ya dakika wafuasi wa Chadema walizidi kuongezeka hali
iliyowalazimisha polisi kuamua kukaa kando.
Msafara huo wa Lowassa uliwasilia kwenye viwanja vya Furahisha saa 9:40 alasiri.
DIALLO, GACHUIMA
Katika hali isiyo ya kawaida jana kutwa nzima kulizagaa taarifa kuwa
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo na Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Wilaya ya Tarime, Christopher Gachuma,
wangerejesha kadi za CCM na kujiunga na Ukawa.
Hata hivyo, viongozi hao hawakujitokeza kama ilivyokuwa imeelezwa
awali ambako umati wa wananchi ulikuwa ukisubiri kwa hamu kuwaona.
MBOWE NA MADAI MAPYA
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
alidai anazo taarifa za kuwapo maofisa watatu ambao ni wataalamu wa
kompyuta waliopelekwa kufanya kazi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
katika mashine za BVR.
Alisema anao ushahidi wa kutosha na kwamba kama kuna mtu anataka ushahidi wa jambo hilo amfuate.
Mbowe alisema maofisa hao wame wamepelekwa NEC kwa masharti ya
kutotambulishwa kama ni askari na wala kutokuvaa sare zao za kazi.
“Siwezi kutaja majina ya maofisa hawa sisi tumekuja kumtambulisha
mgombea wetu. Ninaziomba mamlaka zinazohusika kuacha kuchezea nguvu ya
umma, zikijaribu zitakutana nayo,” alisema.
Bila kumtaja jina, Mbowe alisema yupo mtu aliyetamka kuwa Tanzania
haiwezi kuongozwa na Rais kutoka mikoa ya kaskazini na kuonya kuwa
ukabila wala udini hauna nafasi kwa sasa.
“Kuna kauli iliyowahi kutolewa na kijana mmoja mpumbavu, siwezi
kumtaja jina hapa kwa vile nitakuwa namuongezea umaarufu. Anasema nchi
hii kamwe haitaweza kutawaliwa na mtu kutoka kaskazini, tuna makabila
zaidi ya 150 hapa nchini… hatutamchagua mtu kwa usukuma wake wala umasai
wake, tutamchagua mtu kwa vigezo,” alisema.
Mbatia kushtaki CCM
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema
anatarajia kuwafikisha baadhi ya viongozi wa CCM na jeshi la polisi
katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya Makosa ya Jinai (ICC)
Uholanzi, Novemba mwaka huu.
Alisema kwa sasa anaorodhesha matendo yote ya jinai wanayotenda kwa ajili ya kuwafikisha huko.
Alisema NEC inapaswa kufanya kikao cha maridhiano na vyama vyote
ikiwa ni pamoja na kuwazuia wakuu wa mikoa na wilaya ambao ni makada wa
CCM kutoingilia shughuli za uchaguzi kwa kutoa amri kwa jeshi la polisi.
Mbatia alisema vyama vya upinzani vinalaani mbinu chafu za
kudhoofisha upinzani na kuonya kuwa kamwe hawako tayari kuona nchi
inaingia katika machafuko yasiyo ya lazima.
Juma Duni Haji
Mgombea mwenza wa Ukawa, Juma Duni Haji, alisema asingeweza
kuzungumza katika mkutano huo kutokana na muda finyu na kuahidi kuwa
atazungumza baada ya kuanza kampeni na hivyo akamuachia Lowassa
azungumze.
Lowassa
Akizungumza katika mkutano huo, Lowassa alisisitiza kuwa anagombea ili kuleta maendeleo.
Alisema ataongoza kwa kuipeleka nchi katika mchakamchaka wa
maendeleo na wale wasioweza kasi yake wampishe huku akionyesha
masikitiko yake kwa jeshi la polisi kuwazuia wananchi kufika katika
mikutano yake kwa kuwapiga mabomu.
“Nilisema Arusha na leo nasisitiza hapa Mwanza, tutawaburuza ICC
viongozi wote ambao wanakiuka haki za binadamu. Wanapaswa kutenda haki
kwa vyama vyote na kuacha upendeleo na kuwapiga wananchi bila sababu
yoyote,” alisema.
Aliwapongeza wananchi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla kwa kumpa
mapokezi ya heshima na kueleza kuwa akifanikiwa kuchaguliwa atatatua
matatizo ya barabara, usafiri wa meli na kufufua viwanda ili
wananchi waweze kupata ajira.
“Najua mliahidiwa meli ziwa Victoria, machinga complex, uwanja wa
ndege wa kimataifa wa Mwanza, pia nitaboresha reli ya kati. Mkinichagua
nitahakikisha natekeleza yote haya kwa vitendo,” alisema.
MASHA
Akizungumza katika mkutano huo, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani,
Lawrence Masha, alisema amerudi nyumbani akiwa na dhamira moja ya
kuhakikisha taifa linakombolewa.
Alisema kwa kukishirikiana na wakazi wa Mwanza, Oktoba mwaka huu ukombozi utakamilika.
MGEJA
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja, alisema
mwaka 2005 aliangushwa na James Lembeli katika kura za maoni Jimbo la
Kahama lakini hakufikiria kuhama chama.
“Kama nilishindwa na James Lembeli mwaka 2005 kura za maoni sikuhama
vipi leo nihame kwa kuwa mwanangu ameangushwa kura za maoni? Sikuhama
kwenye nafasi ya vijana.
“Nataka kuwaeleza Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye na
Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana wanaotuita ‘makapi’ kuwawanapaswa
kutambua hayo makapi ni bora sana kwa maana yanafua umeme,” alisema.
Alisema viongozi na wanachama wa CCM kote nchini wanapaswa kujiandaa
kisaikolojia kwa vile Ukawa utaingia madarakani na kuunda serikali ya
awamu ya tano.
“Ukiona nyumba inaungua usisubiri kuambiwa uondoke, niliamua kuondoka
CCM kwa ridhaa yangu. Nilipokea simu zaidi ya 800 zikipongeza kuondoka
kwangu CCM lakini ni simu sita pekee zilizonipigia wakisikitika… wana
CCM waliobaki waondoke,” alisema.
Machemli aibuka:
Naye aliyekuwa Mbunge wa Ukerewe, Salvatory Machemli (Chadema) jana aliibuka na kukana kukihama chama hicho.
Wiki iliyopita Machemli alidaiwa kuhamia Chama cha ACT Wazalendo,, lakini jana alikana akisema hana mpango huo.
“Leo hapa mnaniona sasa niwaulize hapa ni ACT Wazalendo au Ukawa.
Siwezi kuhama bado niko Chadema, siwezi kuhamia chama chochote ndiyo
maana niko hapa leo hii,” alisema.
Habari imeandikwa na John Maduhu, Peter Fabian na Judith Nyange.
Home
News
Mafuriko ya mwanza kwa LOWASSA yatengeneza historia Mpya*Mabomu ya machozi yatawala*Wanachi wawangangari kukabili vishindo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment