Kuanzia wasanii, viongozi wa kisiasa, wakuu wa taasisi na idara mbalimbali na hata wananchi wa kawaida wamekuwa wakikumbana na athari hizi zitokanazo na taarifa potofu zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Hakika, hili ni tatizo. Ni kero kubwa kwa jamii ambayo ni dhahiri
kuwa ikiachwa iendelee kama ilivyo sasa, ni wazi kwamba taifa linaweza
kupata madhara makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Sisi tunalaani
matumizi haya mabaya ya mitandao ya kijamii.
Tunaamini kwamba sasa ni wakati muafaka kwa wananchi wote kuungana
na vyombo vya usalama katika kupambana kila uchao dhidi ya matumizi
mabaya ya mitandao hii. Kadri inavyofahamika, kuwapo kwa mitandao hii
ya kijamii kama ya facebook, twitter, instagram na blogu mbalimbali kuna
manufaa makubwa. Ni kwa sababu uwapo wake unatokana na matunda ya kukua
kila uchao kwa teknolojia ya habari na mawasiliano. Hali hii hutoa
fursa ya kuwaweka karibu zaidi watu wa mataifa mbalimbali.
Kupitia mitandao ya kijamii, dunia sasa imekuwa kama kijiji.
Kinachotokea eneo moja la uso wa dunia kinawafikia wengine walio katika
ncha tofauti ya dunia kwa haraka, uhakika na ubora wa kiwango cha juu.
wa mfano, kupitia kukua huku kwa teknolojia ya habari na mawasiliano,
sasa ni rahisi zaidi kwa wakulima walio katika kijiji ‘A’ kinachotegemea
kilimo kama njia kuu ya uchumi kupata taarifa za soko la mazao yao.
Hili huwezesha biashara kufanyika kwa ufanisi na mwishowe kukuza
uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Na huu ni mfano mdogo tu
wa faida za kukua huku kwa teknolojia ya habari na mawasiliano
kunakowezesha watu kupashana habari kupitia mitandao mbalimbali ya
kijamii. Hata hivyo, inafahamika kuwa palipo na faida, hasara huwa
hazikosekani. Mitandao hii ya kijamii huwa na athari nyingi hasi pindi
isipotumika vizuri. Kwa bahati mbaya, taifa letu lingali likikabiliwa na
tatizo hili la matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
Baadhi ya watu husambaza taarifa za uongo zinazoibua hofu na
mfarakano. Wengine hutoa taarifa zinazotishia usalama wa taifa. Amani na
utulivu huwa shakani. Zipo pia taarifa zinazopotosha umma kuhusiana na
masuala ya afya. Mambo yote haya hayavumiliki hata kidogo.
Mifano kuhusiana na matumizi mabaya ya mitandao iko mingi.
Mathalan, katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika
Oktoba 25, baadhi ya watu wamekuwa wakisambaza taarifa nyingi potofu.
Mmoja wa waathirika wa vitendo hivi katika siku za hivi karibuni ni
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Ghalib Mohamed
Bilal. Wasambazaji wa taarifa potofu walieneza uvumi kupitia mitandao ya
kijamii kuwa kiongozi huyu wa juu amekihama chama chake tawala (CCM) na
kuhamia upinzani.
Hali hii haipendezi hata kidogo. Kwa sababu hiyo, sisi tunadhani
kwamba kuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba vitendo hivi
vinadhibitiwa. Vikiachwa vinaweza kuibua mfarakano kila uchao katika
jamii. Na tunatambua kuwa hii siyo kazi ndogo. Hata hivyo, inawezekana
kudhibiti hali hii ikiwa kampeni endelevu za kuelimisha jamii kuhusiana
na matumizi ya mitandao ya kijamii itafanyika bila kuchoka. Vyombo vya
dola viendelee kuimarishwa kadri inavyowezekana, hasa katika idara zao
za mawasiliano ili mwishowe kupunguza athari za matumizi mabaya ya
mitandao ya kijamii.
0 comments:
Post a Comment