SIKU moja baada ya Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Mabere Marando kukaririwa akisema atatangaza matokeo ya
uchaguzi kabla ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kufanya hivyo, Tume
hiyo imesema anataka kuleta vurugu nchini.
Vilevile, NEC imewaonya wanasiasa kuacha kuingilia kazi zake na
badala yake wafanye kazi zao za kunadi wagombea wao katika majukwaa.
Marando alitoa kauli hiyo juzi jijini Dar es Salaam kwa niaba ya
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao umempendekeza Edward Lowassa
kuwania urais kupitia Chadema.
Ukawa ni muungano wa vyama vinne, Chadema, NCCR-Mageuzi, National League for Democracy (NLD) na Chama cha Wananchi (CUF).
Mkurugenzi wa NEC, Kailam Ramadhan aliliambia gazeti hili Dar es
Salaam jana kuwa mwenye mamlaka ya kutangaza matokeo ni Tume pekee yake
na kuwataka wanasiasa, akiwemo Marando kuwa makini na kauli zao ili
zisilete machafuko nchini.
Ramadhan alisema umakini kwa wanasiasa unahitajika sana hasa katika
kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu. Mkurugenzi huyo alisema matokeo yote
yatatangazwa na Tume au mtu yeyote endapo watamkasimisha, hivyo
wananchi wasisikilize maneno ya wanasiasa.
Alisema Tume imepewa mamlaka kisheria kutangaza matokeo ya uchaguzi
ya udiwani, ubunge na urais kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na
wabunge na siyo vinginevyo.
“Sasa hao wanaosema watatangaza matokeo ya uchaguzi katika kila kituo
watakuwa wanafanya mambo kinyume cha sheria labda watangaze matokeo ya
chama chao, kwani hicho wanachotaka kufanya ni kuleta vurugu katika
uchaguzi,” alisema.
Ramadhan alisema watu wasifikiri sheria hiyo ni ya NEC, kwani
ilipitishwa na wabunge na wanasiasa wenyewe wanafahamu, hivyo hadi
dakika ya mwisho wenye mamlaka ya kutangaza matokeo ni Tume yenyewe.
Aliwataka wanasiasa kufuata sheria na wananchi wasibabaishwe na kauli
hizo, kwani NEC ndiyo yenye mamlaka na kama wanaona sheria hiyo si
sahihi waende bungeni kubadilisha.
Marando alitoa kauli hiyo juzi jijini Dar es Salaam baada ya Lowassa
kumtaka kutoa ufafanuzi wa madai kuwa shahada za kura za askari polisi
na askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) zinakusanywa na viongozi
wao.
Kutokana na hali hiyo, Marando alisema njama zote zinazotumiwa na
Chama Cha Mapinduzi (CCM) za kutaka kuhujumu matokeo, zikiwamo za
kukusanya shahada za polisi na wanajeshi wamezigundua na wamepanga
kuzikabili.
“Njama zote walizonazo kutaka kujaribu kuhujumu kura za Lowassa,
wabunge na madiwani pamoja na kuhujumu kura za Zanzibar tutazidhibiti,
nawaambia mawakala baada ya kupiga kura tu msisubiri saa 12.00 jioni,
nitumieni saa 7.00 mchana nitatangaza matokeo, mheshimiwa usiwe na
wasiwasi, endelea na kazi yako,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment