KAMATI Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imetengua matokeo ya
majimbo matano kutokana na dosari nyingi zilizojitokeza kwenye mchakato
wa kura za maoni.
Mbali na kutengua matokeo hayo, kamati hiyo iliyokuwa chini ya
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete pamoja na mambo mengine
imeamuru kura hizo zirudiwe katika majimbo hayo kesho.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliwaambia waandishi
wa habari mjini hapa jana kuwa Kamati Kuu imeagiza kura hizo kurudiwa
kutokana na kugubikwa na malalamiko mengi.
Nape alisema Kamati hiyo imeagiza upigaji wa kura hizo za maoni
urudiwe katika majimbo matano ya Busega, Kilolo, Rufiji, Makete na
Ukonga.
“Kamati Kuu imeagiza kurudiwa kwa mchakato huo kutokana na dosari
mbalimbali zilizojitokeza na siwezi kuziweka hadharani ila agizo ni hilo
kura zirudiwe kesho siku ya Alhamis, vinginevyo vikao vinaendelea,”
alisema Nape.
Wakati akifungua kikao hicho, Rais aliwataka wajumbe kufanya kazi
iliyowapeleka Dodoma ambayo wananchi wanaisubiri kwa hamu kubwa ya
kupitia na kupitisha uteuzi uliofanywa katika kura hizo huku kikao hicho
kikiwa na wajumbe 25 kati ya 32.
Busega
Kabla ya Kamati Kuu ya CCM kutaka kura za maoni kurudiwa Jimbo la
Busega lilipo mkoani Geita, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk.
Titus Kamani alikuwa waziri wa 10 wa Serikali kuanguka kwenye kura hizo.
Dk. Kamani ameanguka katika kura hizo baada ya kupata kura 11,829 dhidi ya 13,048 alizopata Dk. Raphael Chegeni.
Akitangaza matokeo hayo hivi karibuni katika ofisi ya CCM Wilaya ya
Busega, eneo la Nyagh’anga, Kata ya Nyashimo, Katibu wa Jumuia ya Wazazi
Wilaya ya Busega, William Bandeke, alisema idadi ya wapiga kura
walikuwa 28,157.
Bandeke alisema kati ya wapiga kura hao, kura 454 ziliharibika na
kura halali zilikuwa 27,700 ambapo Dk. Chegeni alipata kura 13,038 na
kumzidi Dk. Kamani kwa tofauti ya kura 1,109 akifuatiwa na Kibese
Bernard aliyepata kura 2,174.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Dk. Chegeni alisema ushindi
huo umeonesha namna wananchi wa Busega walitaka kudhulumiwa haki yao.
“Mimi niseme tu kwamba katika mchakato wowote kuna kashikashi nyingi,
lakini nasikitika kusema kwamba ndani ya chama chetu kuna watu na
mgombea mwenzetu waliamua kuchakachua matokeo,” alikaririwa akisema Dk.
Chegeni.
Kilolo
Kwa mujibu kikao cha Kamati Kuu ya CCM mchakato wa kura za maoni
katika Jimbo la Kilolo lililopo mkoani Iringa unatakiwa pia kurudiwa.
Katika mchakato uliofanyika awali, Venance Mwamoto alipata kura
11,200 wakati Profesa Peter Msolla akipata kura 10, 014 ambapo aligomea
kusaini matokeo.
Akitangaza matokeo hayo usiku, Katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo,
Clemence Mponzi alisema katika uchaguzi huo uliokuwa na wagombea 15,
Mwamoto ni mshindi.
Kuhusu Profesa Msolla kugomea matokeo, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa,
Hassan Mtenga alikaririwa akisema kitendo hicho hakizuii vikao vya
kamati ya CCM ngazi ya mkoa na wilaya kufanyika na kwamba matokeo
hayawezi kubadilishwa wala uchaguzi kurudiwa.
Rufiji
Jimbo la Rufiji nalo liligubikwa na utata mkubwa katika kura hizo za
maoni ambako kamati hiyo imetengua matokeo na kuamuru urudiwe.
Matokeo katika jimbo hilo yaligubikwa na utata na kulazimu Kamati ya
Maadili na Usalama ya CCM Wilaya Rufiji kukutana na iliridhia na
kupitisha matokeo ya kura hizo kwa mbunge wa jimbo hilo anayemaliza muda
wake, Dk. Seif Rashid kupata kura 3,831.
Mgombea aliyefuatia kwa karibu katika matokeo hayo alikuwa Mohamed Omary Mchengelwa aliyepata kura 3,560.
Matokeo yalilazimika kutolewa na kamati hiyo kutokana na kuwepo utata
mkubwa uliosababisha Katibu wa Wilaya ya Rufiji, Mussa Lwalilo
kushindwa kuyatangaza.
Kutokana na hali hiyo, kamati ilikusanya upya matokeo yote katika
kata 13 za jimbo hilo ambazo ni Mgomba, Ikwiriri, Umwe, Mohoro, Chumbi,
Mwaseni, Kipugira, Ngorogo, Mkongo, Utete, Mbwara, ChemChem na Ngarambe
ili kujiridhisha.
Akitangaza matokeo hivi karibuni, Katibu Mwenezi wa Wilaya ya Rufiji,
Mussa Mnyeresi alisema kamati hiyo ilibaini udanganyifu mkubwa
uliofanywa na watumishi wa chama hicho.
Wagombea wengine waliojitokeza katika mchakato huo ni Kamanda Jamali
Rwambow, Shaban Matwebe, Dk. Seif Hassan Sule, Juma Kiobebele, Mohamed
Afif na Tano Mwela.
Makete
Kamati Kuu ya CCM imefuta pia matokeo ya kura za maoni katika Jimbo
la Makete. Katika mchakato huo, Dk. Norman Sigala aliibuka mshindi na
kumbwaga Dk. Binilith Mahenge.
Ukonga
Katika hatua nyingine, Kamati Kuu imetengua matokeo ya Jimbo la
Ukonga lililopo Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam baada ya
kutoridhishwa na namna mchakato huo ulivyofanyika.
Katika mchakato huo, Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa aibuka
kwa kupata kura 10,000, Ramesh Patel 7,356 na Robert Masegese kura 548.
Mchakato wa kura za maoni kwa CCM ulifanyika kuanzia Agosti Mosi, na
kuacha majeraha kwa viongozi wa juu baada ya kuanguka licha ya kuwa na
nafasi nyeti serikalini.
Mawaziri
Mawaziri ambao walianguka katika mchakato huo ni Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe wa Jimbo la Nachingwea aliyepata kura 5,
128 na Hassan Masala kupata kura 6,494.
Mbali na Chikawe, yumo Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka na
manaibu mawaziri. Manaibu walionguka ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim, Naibu Waziri wa Mambo ya
Ndani, Perera Ame Silima na Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla.
Wengine ni Naibu wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Saningio Ole
Telele, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga, Naibu
Waziri wa Fedha, Adam Malima, Naibu Waziri wa Maendeleo, Jinsia na
Watoto, Dk. Pindi Chana.
Mahadhi alianguka Jimbo la Paje, Zanzibar kwa kupata kura 1,785 huku
Jaffar Sanya ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu Mkoa wa Kusini akiibuka
mshindi wa kura 3,368. Silima alyepata kura 1, 218 Jimbo la Chumbuni
alibwagwa na mpinzani wake, Ussi Pondeza kura 1,952.
Home
News
KAMATI Kuu (CC) imetengua matokeo*Majimbo matano kurudiwa kura za maoni *Yabaini madudu lukuki, vigogo kuchuana upya
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment