Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi kutoka Ofisi ya Taifa ya
Takwimu Morrice Oyuke (Kulia) akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar
es Salaam wakati akitangaza matokeo ya takwimu za Pato la Taifa kwa robo mwaka
ya kwanza kuanzia mwezi Januari – Machi, 2015 ambayo yameonyesha kuwa thamani
ya Pato la imekua na kufikia shilingi trilioni 21.9 ikilinganishwa na shilingi
trilioni 18.6 ya robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2014. Kushoto kwake
ni Meneja wa Takwimu za Pato la Taifa Daniel Masolwa wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu.
Matokeo ya takwimu za Pato la Taifa
kwa robo mwaka ya kwanza yaani kuanzia mwezi Januari – Machi, 2015 yameonyesha
kuwa thamani ya Pato la Taifa imekua na kufikia shilingi trilioni 21.9
ikilinganishwa na shilingi trilioni 18.6 ya robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2014.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es
Salaam, Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu
Morrice Oyuke amesema takwimu hizo zimetayarishwa kwa kuzingatia
marekebisho ya Takwimu za Pato la Taifa kwa bei za mwaka 2007.
“Pato la Taifa kwa bei za mwaka 2007 katika kipindi
cha robo mwaka ya kwanza linaonyesha kuwa na jumla ya thamani ya shilingi
trilioni 10.6 kwa mwaka 2015 ikilinganishwa na shilingi trilioni 9.9 katika
kipindi kama hicho mwaka 2014”, amefafanua Oyuke.
Oyuke amesema kuwa, Pato hili la Taifa limeongezeka
kwa kasi ya asilimia 6.5 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015
ikilinganishwa na kasi ya asilimia 8.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2014.
Aidha, Oyuke amesisitiza kuwa utayarishaji wa takwimu
za Pato la Taifa hujumuisha shughuli zote za kiuchumi na hivyo hutumika katika
kutathmini, kupanga mipango na kutayarisha sera za kiuchumi.
Baadhi ya shughuli hizo za uchumi ni kilimo na mifugo
ambazo zilikua kwa kasi ya asilimia 2.6 katika kipindi cha robo ya kwanza ya
mwaka 2015 ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa asilimia 3.4 katika kipindi kama
hicho mwaka 2014.
Shughuli za Uvuvi ziliongezeka kwa asilimia 0.9 kwa
robo ya kwanza ya mwaka 2015 ikilinganishwa na asilimia 2.3 kipindi kama hicho
mwaka 2014. Ukuaji huu ulitokana na jitihada za Serikali kuwasaidia wakulima
kwa kutoa ruzuku na maelekezo ya Ma-ofisa Ugani kwa wakulima kama vile kuchagua
mbegu bora yaliyosaidia kuongeza uzalishaji.
Shughuli za Uchimbaji Madini, Mawe na Kokoto
ziliongezeka kwa kasi ya asilimia 0.6 katika kipindi cha robo ya kwanza ya
mwaka 2015 ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa asilimia 19.7 katika kipindi
kama hicho mwaka 2014.
Shughuli za Uzalishaji bidhaa Viwandani zilikua
kwa kasi ya asilimia 5.7 katika kipindi cha robo ya
kwanza ya mwaka 2015 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 8.2 kipindi kama hicho
mwaka mwaka 2014. Kasi ya ukuaji ilitokana na kuongezeka kwa
uzalishaji wa bidhaa za vyakula, vinywaji, tumbaku, nguo, simenti na bidhaa za
kemikali na madawa.
Shughuli nyingine ni pamoja na Uzalishaji nishati ya
umeme na maji ambazo zilikua kwa kasi ya asilimia 10.7 katika kipindi cha robo
ya kwanza ya mwaka 2015 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 10.1 katika kipindi
kama hicho mwaka 2014. Kuongezeka kwa ukuaji wa nishati ya umeme kulitokana na
kuongezeka kwa umeme uliozalishwa kutoka kwenye mitambo inayotumia, maji,
mafuta na gesi asilia.
Shughuli za Fedha na Bima katika kipindi cha robo ya
kwanza ya mwaka 2015 ziliongezeka kwa asilimia 9.1 ikilinganishwa na asilimia
11.2 kipindi kama hicho mwaka 2014.
Shughuli za Ujenzi (ambazo zinajumuisha
ujenzi wa nyumba za makazi na zisizo za makazi; barabara na madaraja; na
shughuli nyingine za uhandisi) katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015
ziliongezeka kwa asilimia 8.8 ikilinganishwa na asilimia 21.4 katika
kipindi kama hicho mwaka 2014.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu ina jukumu la kutayarisha na
kusambaza takwimu rasmi nchini ikiwa ni pamoja na takwimu za Pato la Taifa kwa
robo Mwaka ambazo hupimwa kwa kuangalia thamani ya bidhaa na huduma
zilizozalishwa nchini katika vipindi vya miezi mitatu mitatu ambavyo ni Januari
– Machi, Aprili – Juni, Julai – Septemba na Oktoba -
Desemba.
0 comments:
Post a Comment