KATIKA mtizamo unaohusisha siasa na dola inaelezwa kuwa ni kila kitu
kinachofanywa na dola au Serikali. wasomi kama Mao Tsetung na Otto Von
Bismark wanashikilia msimamo huu.
Udhaifu wa mtizamo huu umeshindwa kuelezea taasisi nyingine kama vile
vyama vya siasa vinaingia kwenye kundi gani kwa kuwa hawavitaji wala
kuvihusisha na siasa kwenye maana waliyoitoa.
Miongoni mwa wasomi wanaofafanua mtizamo huo ni Okwudiba Nnoli na Harold Lasswell.
Nnoli anasema siasa ni mchakato unaohusisha uchukuaji wa nguvu ya
dola, utekelezaji wa madaraka ya dola na ulinzi wa nguvu ya dola.
Lasswell anasema siasa inajikita katika mgawanyo wa rasilimali. Ili mgawanyo huo utokee ni lazima mgawaji awe na nguvu za dola.
Kwa upande wake, Mwanafalsafa Aristotle anasema siasa ni shughuli ya kimaadili inayohusiana na ujengaji wa jamii yenye usawa.
Anaendelea kueleza kuwa binadamu ni mnyama wa kisiasa anayeishi
kwenye jamii ya kisiasa hivyo kila kitu ni siasa. Mimi binafsi naunga
mkono mtizamo huu wa Aristotle
Pia, tafsiri nyingine ya neno siasa ni njia ya kufanya uamuzi katika
taifa, mji au hata dunia nzima. Sehemu muhimu ya siasa ni majadiliano
kati ya watu mbalimbali wenye nguvu au mamlaka.
Katika demokrasia kila mtu ana kiasi fulani cha nguvu, kwa hiyo siasa
ya demokrasia ina maana ya watu wote kuchangia maamuzi, lakini pia
wachache hawapuuzwi.
Aidha, demokrasia ni mfumo wa Serikali, ambapo wananchi wote ni sawa
mbele ya sheria na wanashiriki katika kufanya uamuzi wa kitaifa kuhusu
masuala ya umma.
Wakati mwingine wananchi hushiriki moja kwa moja. Hii ina maana kuwa
wao hupiga kura moja kwa moja kwenye masuala kama vile sheria na katika
chaguzi na wakati mwingine huwakilishwa na viongozi wao waliowachagua.
Kwa Tanzania dhana ya wachache ilikubalika wakati wa mchakato wa
kuruhusu uwepo wa vyama vingi, ambapo asilimia 80 walisema hawakubali na
asilimia 20 wakakubali. Hata hivyo, kutokana na busara ya kisiasa ya
Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mfumo huo uliruhusiwa na
leo unafanya kazi.
Naweza kusema kuna uwezekano mkubwa kuwa haya yanayotokea sasa nchini
yanajikita katika maana hizo ambazo nimejaribu kuzifafanua kuhusu siasa
na demokrasia lakini ukweli utabaki pale pale kuwa ufanisi huo unaacha
makovu kwa baadhi ya watu.
Tanzania ikiwa moja ya nchi ambayo inaendeshwa kwa kufuata misingi
hiyo ya kidemokrasia bado jamii yake imekuwa ikitoa tafsiri chanya na
hasi kuhusu maana ya maneno hayo hivyo kusababisha hali ya sintofahamu.
Ni wazi kuwa kwa dhana hiyo unaweza kuwaona Watanzania wakishiriki
kikamilifu kujadili jambo ambalo kwa mantiki yake wakati mwingine halina
athari kwa nchi na jamii yenyewe.
Hali hiyo wakati mwingine imekuwa ikiharibu au kusababisha mambo
mengine muhimu kutopewa kipaumbele hivyo kuharibika kisa watu wanajadili
jambo fulani ambalo athari yake inaweza kuwa ndogo.
Mfano kitendo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), suala hilo limeweza
kuteka hisia za Watanzania huku dhana ikijikita katika usaliti, tamaa
ya madaraka na kauli nyingine ambazo kisiasa hazikuwa na maana tofauti
na ukweli kuwa wanaojadili hawajui wanachokijadili kisiasa.
Kimsingi nasema hawajui wanachokijadili kwa misingi ambayo nimeieleza
hapo awali, kwani suala la kuhamia au kutohama kwa mtu iwe amekosewa
ndipo akahama au katika siasa majibu yake yatajikita kwenye haki yake ya
msingi na kuwa hiyo ndiyo demokrasia sahihi kwa mhusika.
Jambo la ajabu katika nchi ya Tanzania ni dhahiri kuwa jamii inaweza
kudumu kwenye dhana hiyo kwa kipindi kifupi na tukio husika likipita
jamii inaendelea na mambo mengi hivyo kulisahau tukio la nyuma ambalo
linaweza kuwa liliwaumiza au la.
Baada ya Lowassa kujiunga Chadema na kupitia michakato yote ikiwa ni
pamoja na kuchukua fomu kuliibuka jambo lingine la Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk. Willibrod Slaa, kutoonekana hadharani, ambapo Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe amejitokeza mbele ya vyombo vya habari na kusema
hali hiyo inachangiwa na katibu huyo kutokubaliana na uamuzi wa wengi
kwa ujio wa Lowassa.
Kauli hiyo ya Mbowe inatokea ikiwa ni takribani wiki moja baada ya
kuwepo ming’ono mbalimbali kuwa kiongozi huyo anatarajiwa kuachana na
chama hicho kisa Lowassa.
Iwapo Dk. Slaa ataondoka au kuacha siasa kisa Lowassa nadiriki kusema
kiongozi huyo alipaswa kuwa kanisani hadi sasa kwani kimsingi hajui
siasa kwa misingi ya siasa inavyotaka.
Naamini dhana nzima ya kuwa katika siasa hakuna audui wa kudumu au
rafiki wa kudumu atakuwa hajailewa hivyo ni vema ajifunze ili
kuhakikisha kuwa hii sintofahmu inaondoka kwa jamii ambayo ilikuwa na
uelewa kama wake.
Aidha, iwapo anafanya hayo kwa kukosa nafasi ya kugombea urais pia
ninadiriki kusema yeye ni mbinafsi, kwani angetakiwa kujitokeza katika
mchakato mzima wa kuchukua fomu na kura za wajumbe wa mkutano mkuu ndizo
zingetoa maamuzi.
Siasa zinahitaji uvumilivu na subra lakini pia hazilazimishwi
kutokana na ukweli kuwa wanaochagua ni watu na watu hao huwa wanakuwa na
maamuzi yao binafsi na sio kwa mtu ambaye yeye anataka.
Nadhani neno fursa bado halijaeleweka vizuri kijijini na katika
kuhakikisha kuwa suala hilo linafika katika ngazi zote ni wajibu wa
wahusika kutoa elimu kwa jamii hasa hiyo ambayo inatakiwa kuingia katika
misingi husika.
Dk. unapaswa kujua iwapo unasusia haya ni dhahiri kuwa iwapo ungepata
nafasi ya kushinda urais Watanzania wengi ambao wameshiriki moja kwa
moja katika mikakati yako au wale ambao wanatajwa katika kashfa
mbalimbali wajiandae kukaa mkao wa kuumia kwani hatakuwa na msamaha na
mtu.
Siasa zinahitaji uvumilivu na upendo hivyo ulikuwa unayapinga hayo
kwa nguvu ya umma na sio ushahidi sahihi tambua kuwa umekuwa sehemu
sahihi ya kuangusha Serikali ambayo imekuwa ikitajwa kwa sifa mbalimbali
za kitaifa na kimataifa.
Mabadiliko ya kisiasa yanapaswa kutambulika kuwa hayawezi kuja kwa
furaha ya wachache na wengi wabakie kimya, ni lazima kuwa baadhi ya
wachache waumie kwa maslahi ya wengi.
Mifano ambayo imeonekana katika nchi ya Tanzania na nchi jirani ni
somo tosha la kukabiliana na dhana mgando za kujadili mtu mmoja ambaye
katika ushahidi amefanya vizuri ila anaweza kusababisha aonekane kuwa si
sehemu sahihi ya kukaa kujadili hatma ya nchi yetu.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment