Image
Image

Sunamii-Makongoro Mahanga amfuata Lowassa.

MWANASIASA aliyepata lawama za kulazimisha ushindi katika uchaguzi mkuu wa 2010 jimboni Segerea akigombea ubunge, Dk. Makongoro Mahanga, amejiondoa rasmi Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hapo hapo Mahanga alitangaza nia ya kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).
Mahanga anamfuata Edward Lowassa, ambaye anasubiri tu vikao vya juu kesho kuidhinisha kuwa mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Kwa miaka mingi Mahanga amekuwa akitajwa kama mwanasiasa kijana ambaye ni mfuasi mkubwa wa Lowassa, na ilitazamiwa kuwa hatabaki CCM iwapo ataangushwa katika kura za maoni za kuwania tena ubunge. Inasemekana kuwa kwake mtiifu kwa Lowassa kumemchongea.
“Ninatangaza rasmi kuwa kuanzia leo tarehe 2 Agosti 2015, mimi Makongoro Mahanga si mwanachama tena wa CCM na ninakusudia kujiunga Chadema kama kitakubali kunipokea,” amesema mbele ya vyombo vya habari leo.
Mahanga ambaye alikuwa naibu waziri wa kazi, ametoa tamko hilo saa chache baada ya kuthibitika rasmi kuwa ameangushwa katika kura za maoni za kutafuta mgombea wa CCM kugombea ubunge jimbo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi jimbo hilo, Mahanga ameshindwa kwa kura na Mama Kevella, ambaye ni mke wa mkurugenzi wa Yono Auction Mart, atakayesubiri uteuzi kufanywa na ngazi ya juu ya CCM.
Katika hali iliyoonesha ukubwa wa tatizo la uchafuzi wa taratibu linalolaumiwa kukithiri ndani ya mfumo wa CCM, Mahanga alisema amechukizwa na wizi wa kura uliofanywa wakati wa uchaguzi huo.
“Nawataka pia wanachama wengine wa CCM ambao hawakufurahishwa na wizi wa kura uliofanyika, waungane nami kujiunga na Chadema,” amesema mbele ya waandishi wa habari aliokutana nao nyumbani kwake, Plot 1071, Kitalu S, Segerea mwisho, Dar es Salaam.
Matokeo yaliyomuangusha Mahanga, ni muendelezo wa vipigo vilivyowakumba viongozi maarufu wa CCM katika kura za maoni zilizofanyika nchini kote jana, wakiwemo mawaziri serikalini.
Kitendo cha Mahanga kuomba kupokewa Chadema, kinaashiria kuwa yupo tayari kufuata masharti ya Chadema kukaribishwa kuwa mwanachama mpya. Aidha, anahitimisha fununu zilizokuwa zimeenea kuwa amekubali kuhamia Chadema, bila ya kutarajia kupewa nafasi ya kugombea ubunge jimbo hilo, hasa kwa kuwa tayari kuna waombaji waliopigiwa kura kwa ajili hiyo.
Segerea ni moja ya majimbo ya mkoani Dar es Salaam ambayo hayajafanyiwa uamuzi wa chama kipi kati ya vyama vilivyoungana chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kitagombea.
Chama cha Wananchi (CUF) kimemteua naibu katibu mkuu wake wa zamani, Julius Mtatiro kugombea ubunge jimbo hilo. Miongoni mwa washindani wake Mtatiro katika kura ya maoni CUFa, ni Ashura Mustafa, aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari Taifa.
Chadema pia kiliendesha kura ya maoni kwa waombaji wake.
Vyama vya UKAWA vimeisulubu ngome ya CCM katika jimbo hilo kwa kutwaa zaidi ya asilimia 70 ya viti vya serikali za mitaa katika uchaguzi wa kitaifa wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji uliofanyika nchini kote Desemba mwaka jana. Chadema ilitwaa viti 14 na CUF viti 11 katika jimbo hilo.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment