PAMOJA na kampeni za kisiasa za kuwania dola kuanza kwa kishindo
nchini, kuna baadhi ya makundi ya watu yamekuwa yakitumia maneno
mbalimbali kupotosha ukweli ambao umetamkwa katika moja ya muktadha ya
mikutano ya kampeni.
Ingawa kazi ya kila chama cha siasa kilichoundwa nia yake ni kukamata
dola na kutekeleza fikira zake, vitendo vinavyofanyika kupotosha maneno
na kuyashupalia ni kitendo kinachoonesha udhaifu katika kunadi sera.
Ni vyema kama makundi hayo yakatambua ukweli wa ubaya wa kushupalia
na kupotosha ukweli wa mambo kwa manufaa yao binafsi, ili kupata
’kicheko’ kisichostahili kwa hila na ghilba.
Pamoja na upotoshaji mkubwa wa mwenendo wa taifa hili tangu
kuanzishwa rasmi kwenye miaka ya sitini, kauli zinazoyumbisha maana
halisi ya mambo inatia kichefuchefu na ni vyema wahusika wakaachana na
kauli hizo za kupotosha.
Hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi,
Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alisema juu ya dhana
potofu ya ukombozi inayoshadidiwa na baadhi ya vyama na wagombea wao,
huku kiukweli kazi hiyo ya ukombozi ikiwa imeshafanywa na waasisi wa
taifa hili Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Karume.
Akiwa anatambua kwamba watu wanaofanya kelele hizo, za kudai ukombozi
wakati nchi ilishakombolewa, ni watu ambao wanafanya hivyo kwa malengo
ya kibinafsi, aliwakumbusha Watanzania kwamba kazi ya ukombozi imefanywa
miaka ya 60 na ASP na Tanu wakati huo na kusema kudai kuwa ukombozi
haujafanyika ni kauli ya dharau kwa Watanzania na waasisi wa taifa hili.
Na katika kuimarisha usemi wake, alisema wazi kwamba wanaodharau
ukombozi uliofanywa na vyama hivyo ni wapumbavu na malofa, tena bila
kumtaja mtu alikuwa anasema wazi kuhusu dharau ya kazi iliyofanywa na
wazee wa taifa hili.
Haiwezekani kwa watu wenye akili timamu, wanaojua mambo, kusema
kwamba taifa hili halijakombolewa na kushawishi vijana ambao sasa ni
wengi kudharau historia na kuanzia pale historia inapokoma.
Pamoja na kushupalia kwamba ni kauli ya matusi, ukweli unabaki
palepale kwamba hayo si matusi, ni maneno yanayoonesha dhahiri uwapo wa
watu ambao wanajua lakini wanakwepa ukweli huo wa kihistoria na hawa
lazima wawe wapumbavu ambao tafsiri yake ni mazuzu na majuha tu.
Na hakuna shaka kabisa watu hao ni malofa, si wa fedha, bali wa
umasikini wa uelewa na wamekuwa watu kupayapaya. Tunachotaka kusema hapa
maneno ya ukweli yasitumike vibaya kwani kwa muktadha wake Rais wa
awamu ya tatu alikuwa sahihi kutokana na uchambuzi wa mambo ambao
aliufanya.
Tufanye siasa kwa kuzingatia ukweli lakini si kwa kuyumbisha wananchi
na kutumia vibaya maneno ambayo yanastahili kutumika kwa wakati huo.
Tukumbuke kwamba Rais mstaafu Benjamin Mkapa alikuwa mhariri katika
gazeti makini na mahiri na anajua uchaguzi wa maneno na mahali muafaka
wa kuyazungumzia na hivyo wananchi wasipotoshwe.
Ni kweli kabisa, katika hili Rais mstaafu hajatukana, bali amewaambia
watu wasiokuwa na busara na wanaodharau historia ya nchi waache
kuwapotosha wengine kwani wanajua kiundani wanayosema si sahihi.
Ni matumaini yetu kwamba wanasiasa wanaowania kuingia Ikulu
hawatasita kuzungumza ajenda zao na kukumbuka historia ya nchi hii
ambayo imetufikisha katika mahali pa kuweza kunadi sera za maendeleo na
si kudharau historia.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment