TIMU ya Taifa Tanzania ya Wanawake (Twiga Stars) inatarajiwa kuingia
kambini leo kisiwani Zanzibar kujiandaa na Michezo ya Afrika (All Africa
Games) itakayofanyika mwezi ujao nchini Congo Brazzaville.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto
alisema kuwa kikosi hicho kitakuwa na wachezaji 25 chini ya kocha wao
mkuu, Rogasian Kaijage. Alisema kuwa kikosi kinaendelea na mazoezi
kujiandaa na michezo hiyo, ambapo Tanzania ilikata tiketi ya kushiriki
fainali hizo baada ya kuiondoa Zambia kwa kuifunga jumla ya mabao 6-5.
Awali, timu hiyo ilikuwa imepiga kambi Mbande huku wenzao wa Taifa
Stars wakitafutiwa kambi nje ya nchi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo
dhidi ya Nigeria utakaofanyika baadae mwezi ujao.
Taifa Stars iko katika kampeni za kufuzu kucheza fainali za Mataifa
ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Gabon 2017 na tayari imeshafungwa na
Misri katika hatua ya makundi. Kizuguto alisema Twiga Stars inaingia
kambini kwa gharama za TFF, huku jitihada za TFF kuwasiliana na Kamati
ya Olimpiki Tanzania (TOC) zikiendelea kuona ni jinsi gani kamati hiyo
inaihudumia timu hiyo ya Taifa kwa ajili ya maandalizi ya michuano hiyo.
TFF inatambua kuwa TOC ndio wana jukumu la kuhudumia timu za Taifa
kuelekea kwenye michuano hiyo ya Michezo ya Afrika, ikiwemo Twiga Stars.
Twiga Stars ambayo imefuzu kwa fainali za Michezo ya Afrika itakayoanza
kutimua vumbi Septemba 04 – 17 imepangwa kundi A pamoja na wenyeji
Congo Brazaville, Nigeria pamoja na Ivory Coast.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment