HATIMAYE kiungo na nahodha wa FC Platinum ya Zimbabwe, Thabani
Kamusoko ametua jijini Dar es Salaam jana kwa ajili ya kusaini mkataba
wa kujiunga na Yanga. Kamusoko alipokewa na Meneja wa Yanga, Hafidh
Saleh jioni kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA), ambapo alipelekwa katika kikao na uongozi kwa mazungumzo.
Akizungumza uwanjani hapo baada ya kutua mchezaji huyo, alisema
amekuja kikazi zaidi na Yanga hawatajutia kumsajili endapo watafikia
makubaliano. Kamusako aliyewahi pia kuchezea Dynamos FC ya Zimbabwe,
anatarajia kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Yanga.
Mchezaji huyo rasta aliyeivutia Yanga ilipokutana na FC Platinum
katika Kombe la Shirikisho mwanzoni mwa mwaka huu, anatarajia kuziba
nafasi iliyoachwa wazi na Mghana Kpah Sherman aliyeuzwa Mpumalanga Black
Aces ya Afrika Kusini.
Lakini pia, Yanga iko mbioni kuwaacha wachezaji wake wengine wawili
wa kigeni, beki Mghana Joseph Tetteh Zutah na kiungo Mbrazili Andrey
Coutinho. Dirisha la usajili Tanzania Bara linatarajiwa kufungwa saa
6:00 usiku leo huku ikibaki nafasi ya kuwasajili wachezaji huru pekee.
Baada ya Yanga kutolewa katika robo fainali michuano ya Klabu Bingwa
Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, imekitathmini kikosi chake na
kugundua Zuttah na Coutinho hawana faida.
Coutinho alijiunga na Yanga SC msimu uliopita akiletwa na aliyekuwa
kocha wa timu hiyo, Mbrazili mwenzake, Marcio Maximo na hadi sasa
ameichezea timu hiyo mechi 33 na kuifungia mabao sita.
Mbrazili huyo alikuwa ana wakati mzuri chini ya kocha Maximo, lakini
tangu ujio wa Mholanzi, Hans van der Pluijm hana namba ya kudumu katika
kikosi cha kwanza cha timu hiyo. Zuttah amesajiliwa Juni mwaka huu
kutokana na kupendekezwa na kocha Pluijm, lakini baada ya wiki mbili za
Kombe la Kagame, uongozi umeona hana umuhimu.
Mbali na Sherman, Coutinho na Zuttah, wachezaji wengine wa kigeni
waliopo Yanga ni Mkongo Mbuyu Twite, Mnyarwanda Haruna Niyonzima, Mrundi
Amissi Tambwe na Mzimbabwe Donald Ngoma.
Yanga SC ilifungwa kwa penalti 5-3 baada ya sare ya 0-0 ndani ya
dakika 90 katika robo fainali ya Kagame dhidi ya Azam FC wiki iliyopita
na tathmini ya baada ya mashindano, inaonesha timu inahitaji marekebisho
kadhaa.
0 comments:
Post a Comment